• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
Waziri wa Ulinzi Ethiopia akana tetesi jeshi limetwaa mamlaka

Waziri wa Ulinzi Ethiopia akana tetesi jeshi limetwaa mamlaka

Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia, Bw Siraj Fegessa. Picha/ Hisani

Na MASHIRIKA

ADDIS ABABA, ETHIOPIA

WAZIRI wa ulinzi wa Ethiopia alikanusha habari kwamba jeshi lilitwaa mamlaka, siku moja baada ya nchi hiyo inayokumbwa na mzozo wa kisiasa kuwekwa chini ya hali ya hatari.

Hata hivyo, waziri huyo Siraj Fegessa, alipuuzilia mbali uwezekano wa kubuniwa kwa serikali ya mpito siku mbili baada ya kujiuzulu kwa waziri mkuu Hailemariam Desalegn.

Bw Desalegn anaendelea kushikilia mamlaka baada ya kutangaza siku ya Alhamisi kwamba alikuwa amewasilisha barua ya kujiuzulu ili kusaidia mageuzi ya kisiasa yaliyopangwa katika moja ya nchi za Afrika zilizo na uchumi unaoendelea kustawi.

Hali ya hatari iliyotangazwa Ijumaa itadumu kwa miezi sita na kuna uwezekano wa kuongezwa kwa miezi minne zaidi sawa na hali ya hatari ya awali.

Hali hiyo mpya ya hatari, ambapo maandamano yamepigwa marufuku, itawasilishwa kwa wabunge ili kuidhinishwa katika muda wa siku 15.

Saraj alisema kuwa maafisa wa usalama wameagizwa kuchukua hatua dhidi ya wanaosumbua nchi huku mahakama maalumu ikianzishwa kushughulikia kesi zao.

Mnamo Ijumaa, baraza la mawaziri lilitaja vifo, mashambulio ya kikabila na kufurushwa kutoka makao kwa watu kama sababu za kuwekwa kwa hali mpya ya hatari.

 

Maandamano

Tangazo hilo lilijiri baada ya maandamano yaliyolemaza shughuli katika miji iliyoko jimbo la Oromia Jumatatu na Jumanne kutaka wafungwa wa kisiasa waachiliwe huru na kushinikiza serikali ifanye mageuzi.

Maandamano kama hayo yalifanyika Ethiopia 2015, na kufanya serikali kutangaza hali ya hatari mnamo Oktoba 2016 baada ya mamia ya watu kuripotiwa kuuawa. Mkanyangano uliotokea katika mkutano wa kidini kusini mashariki mwa Addis Ababa mwezi huo ulisababisha vifo vya watu wengi.

Kutokana na hali hiyo ya hatari, watu zaidi ya 22,000 walikamatwa na biashara nyingi kuathiriwa.

 

‘Kupewa mafunzo’

Makundi ya kutetea haki za binadamu yanadai kwamba watu walipigwa na kuzuiliwa kiholela. Serikali ilisema kwamba waliokamatwa kimakosa waliachiliwa huru na wale walioshiriki kwenye maandamano waliachiliwa baada ya kile ilichotaja kama kupewa mafunzo.

Amerika imeonya wafanyakazi wa ubalozi wake nchini Addis Ababa kusitisha safari zote nje ya jiji kuu.

Na shirika la habari la taifa la Fana liliripoti kuwa balozi wa Amerika katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, alikutana na kujadili mzozo wa sasa wa kisiasa nchini Ethiopia na waziri wa mashauri ya kigeni Workneh Gebeyehu jijini New York.

Mwanablogu maarufu Befekadu Hailu, aliyefungwa jela kwa sababu ya habari za kukosoa serikali, ameitaka serikali ya Ethiopia kufanya mageuzi ya kweli, kujadiliana na makundi halali ya upinzani na kuandaa nchi kwa uchaguzi huru na wa haki ili kutatua mzozo wa sasa.

 

 

You can share this post!

ADUNGO: Hakika mtu yeyote anayetaka kushabikia Arsenal...

Manusura akejeli Trump kwa kuzembea kudhibiti umiliki wa...

adminleo