• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:36 PM
TAHARIRI: Wakuu KNH watoe huduma ipasavyo

TAHARIRI: Wakuu KNH watoe huduma ipasavyo

Kitengo cha huduma za dharura za matibabu cha Hospitali Kuu ya Kenyatta. Picha/ Maktaba

KWA mara ya pili sasa Hospitali Kuu ya Kenyatta aimejipata ikizungumzwa na Wakenya, kutokana na jinsi inavyoshughulikia masuala ya usalama wa wagonjwa.

Wiki chache zilizopita, kulikuwa na madai ya kuwepo visa vya kuvamiwa wanawake waja wazito na watu waliokuwa na dhamira ya kuwabaka. Wakati huo ilidaiwa kuwa wanawake hao wamekuwa wakiingia ndani ya lifti zenye giza.

Usimamizi wa hospitali hiyo kubwa zaidi nchini ulikanusha madai hayo, na kufikia leo haijafahamika kama kweli kisa hicho kilikuwa ni ukweli au la.

Kinachoudhi ni kwamba, punde baada ya kuiuka madai hayo, wakuu wa hospitali hiyo walibadilisha walinzi na kudai kuwa usalama katika KNH utakuwa wa hali ya juu, lakini mambo ni tofauti kabisa.

Usiku wa Jumapili, kuliripotiwa kisa cha kuibwa kwa mtoto katika hospitali hiyo. Ilisemekana kuwa mtoto huyo, Prince, aliibwa katika eneo la watu kusubiri kuhudumiwa.

Babake mtoto huyo aliyezaliwa pacha wiki mbili zilizopita, Bw Job Nyatiti Ouko, alisema alikuwa amempeleka mkewe katika KNH akiwa na matatizo ya moyo, na kuwabeba pacha wake ila hakujua angekabiliwa na masaibu zaidi.

Wakiwa hospitalini, Bw Ouko na mkewe walianza kuzungumza na mwanamke aliyekuwa ameandamana na mwanamke mwingine. Kwa vile walikuwa wakiongea lugha ya kwao, mtu na mkewe waliamua kuwaachia watoto wao kuwaangalilia, huku wakishughulika na kumwona daktari.

Baada ya muda mfupi, mmoja wa wanawake alikimbia chumbani walimokuwa na kuwafahamisha kuwa mwanamke yule mwingine alikuwa ametoroka na mtoto mmoja.

Kamera za CCTV KNH zilimnakili mwanamke aliyeshukiwa kuiba mtoto huyo, dakika chache kabla ya kupanda bodaboda na kutokomea. Lakini wakuu wa KNH walionekana kutokuwa na habari au kutaka suala hilo lichukuliwe kuwa la kujitakia.

Hospitali ya Kenyatta ni ya rufaa na hutumiwa zaidi na idadi kubwa ya Wakenya wasiokuwa na uwezo wa kwenda katika hospitali za kibinafsi.

Wananchi hao ndio walipa ushuru na wanastahili huduma bora, ikiwemo kuchunngiwa watoto wao na wao wenyewe. Wakuu wa hospitali ni lazima watekeleze wajibu huo bila visingizio.

 

 

You can share this post!

Nuttal apigwa kalamu Ghana kuhusu ufisadi

Atimua dadake kwa kumvurugia mke

adminleo