• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Geti ya Sh20 milioni Nyeri yaibua maswali

Geti ya Sh20 milioni Nyeri yaibua maswali

MAKAO makuu ya kaunti ya Nyeri ambako imependekezwa lango la sasa libadilishwe na jingine litakalogharimu Sh20 milioni liwekwe. Picha/Grace Gitau

Na GRACE GITAU

Kwa ufupi:

  • Haieleweki kwa nini kaunti hiyo imeamua kujenga geti mpya katika makao makuu, miaka miwili tu baada ya lango hilo kufanyiwa ukarabati
  • Gavana Mutahi Kahiga asema hajui kiwango cha pesa kitakachotumiwa kwani hizo sio hesabu za mwisho
  • Majuzi Gavana Kahiga alinunua gari jipya aina ya Prado lililogharimu Sh14 milioni lakini halikuwa kwenye bajeti ya ziada iliyopitishwa
  • Kaunti hiyo pia imepanga kujenga afisi mpya kwa Sh500 milioni

KAUNTI ya Nyeri imependekeza kutumia Sh20 milioni kujenga lango kuu la makao makuu ya kaunti hiyo.

Kulingana na ripoti ya mipango ya maendeleo katika kipindi cha kifedha cha mwaka wa 2018/2019, kaunti hiyo pia imependekeza Sh200 milioni zitumiwe kumjengea Gavana nyumba rasmi. Kiwango hicho ni maradufu ya kiwango kilichokuwa kimependekezwa na utawala uliotangulia.

Pesa hizo zitatumiwa kununua ardhi, kugharamia malipo ya usanifu na ujenzi wenyewe kuanzia 2018 hadi 2022.

Haieleweki kwa nini kaunti hiyo imeamua kujenga geti mpya katika makao makuu, miaka miwili tu baada ya lango hilo kufanyiwa ukarabati na utawala wa aliyekuwa gavana, marehemu Nderitu Gachagua.

Pesa hizo zinazopendekezwa kujenga geti zinaweza kutosha kuandikisha na kulipia ada ya afya ya NHIF kwa wakazi 3,000 wa Nyeri wasiojiweza na hivyo kuwapunguzia gharama za matibabu.

Hata hivyo, takwimu zilizo kwenye ripoti hiyo ni makadirio ambayo yanaweza kubadilishwa wakati bajeti ya mwisho itakapoundwa.

Kwenye mahojiano kuhusu suala hilo, Gavana Mutahi Kahiga alisema hajui kiwango cha pesa kitakachotumiwa kwani hizo sio hesabu za mwisho.

 

Nyumba

Kulingana naye, hatua ya kutenga pesa za kujenga nyumba za magavana, manaibu wao na maspika ni kutokana na agizo lililotolewa na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC).

“Tume hiyo iliambia serikali za kaunti kuwa magavana, manaibu wao na maspika hawatapokea marupurupu ya nyumba kuanzia Julai 2019,” akasema Bw Kahiga.

Waziri wa Fedha na Mipango ya Kiuchumi katika kaunti ya Nyeri, Bw Robert Thuo, alisema makadirio hayo ni maandalizi ya bajeti kamili.

“Huwezi kunukuu ripoti ya maandalizi. Hakuna bajeti ya nyumba hiyo na hakuna pesa zilizotengwa kwa minajili ya ujenzi wake hadi bajeti itakapopotishwa,” akasema.

Ripoti hiyo huwa ni stakabadhi muhimu inayotoa maelezo ya kina kuhusu miradi ambayo kaunti imepanga kutekeleza katika mwaka wa kifedha. Huwa inafanyiwa uchanganuzi na kuidhinishwa katika bunge la kaunti ambapo madiwani huitumia kuunda bajeti ya mwaka.

 

Gari jipya

Majuzi Gavana Kahiga alinunua gari jipya aina ya Prado lililogharimu Sh14 milioni lakini halikuwa kwenye bajeti ya ziada iliyopitishwa katika bunge la kaunti.

Bw Kahiga alikuwa amelalamika kuwa hana gari rasmi la kikazi na alihitaji gari jipya kwa vile gari aina ya Mercedez Benz lililokuwa likitumiwa na marehemu Wahome Gakuru liliharibika lilipopata ajali.

Kaunti hiyo pia imepanga kujenga afisi mpya kwa Sh500 milioni ambayo imepangiwa kukamilishwa miaka mitano ijayo.

Walipa ushuru pia watagharamia ujenzi wa afisi za wadi na za kaunti ndogo kwa Sh84 milioni, huku kaunti ikipanga kutumia Sh30 milioni kwa ununuzi wa magari ya wasimamizi wa kaunti ndogo.

You can share this post!

Pacha aliyeibwa hospitalini Kenyatta apatikana

Msafara wa Naibu wa Joho washambuliwa kupinga vioski...

adminleo