• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 12:45 AM
Wafuasi wa Ruto wataka Jubilee iandae mkutano

Wafuasi wa Ruto wataka Jubilee iandae mkutano

ONYANGO K’ONYANGO na WYCLIFF KIPSANG

BAADHI ya wabunge wa Jubilee wanaompigia chapuo Naibu Rais, Dkt William Ruto sasa wanataka mkutano wa kundi la wabunge wa chama (PG) uandaliwe ili kutatua masuala tata.

Viongozi hao hapo jana walisikitikia mgawanyiko unaoendelea ndani ya Jubilee hasa kuhusiana na ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) iliyozinduliwa mwishoni mwa mwaka jana.

Wabunge Nelson Koech (Belgut) na Daniel Rono (Keiyo Kusini) sasa wanadai kwamba Rais Uhuru Kenyatta anafaa aitishe mkutano wa PG na ule wa Baraza Kuu (NEC) iwapo kwa kweli anatilia maanani masuala ya chama hicho.

Bw Rono bila kutoa ufafanuzi wa kina, alidai kwamba Rais Kenyatta ametekwa na ukuruba wake kisiasa na kinara wa ODM Raila Odinga kiasi kwamba hana muda wa mambo ya Jubilee tena.

“Mkutano wa NEC ulifaa uwe umeandaliwa kufikia sasa. Rais ametekwa na Bw Odinga na Waziri, Dkt Fred Matiang’i ndiyo maana hawezi kuwakabili wabunge wanaomwambia ukweli. Anachukia kuelezwa ukweli kwa sababu amevunja ahadi nyingi za kisiasa,” akasema Bw Koech.

Aliongeza kuwa kuandaliwa kwa mikutano ya NEC na PG kutakuwa njia bora ya kutatua masuala tata ndani ya chama hicho badala ya kukimbilia viongozi kutoka nje.

“Kuna haja ya kukabili matatizo yetu badala ya kuyahepa kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ambayo chama kinaweza kusalia imara. Tuliunda Jubilee kwa kutumia msingi wa vyama vilivyohudumu kwa muda mrefu kama Chama cha Kikomunisti cha China,” akasema Bw Koech.

Salamu za heri kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga zimetishia kuvuruga umoja wa Jubilee huku viongozi wanaomuunga mkono Dkt Ruto wakisema ushirikiano huo unatumiwa kumhujumu kisiasa.

Kuchipuka kwa makundi ya Tangatanga na Kieleweke ambayo yanaegemea upande wa Rais na naibu wake pia kumechangia mgawanyiko mkubwa ndani ya chama.

Jubilee haijaandaa mkutano wake wa PG kwa karibu miaka mitatu huku Katibu Mkuu Raphael Tuju akinukuliwa na wanahabari akisema ni Rais pekee ambaye ana uwezo wa kuitisha mkutano huo.

“Tunashanga kuhusu mienendo ya Rais wetu. Amekuwa mwenye hamaki kila mara na hii ndiyo maana tunafaa tuwe na PG au NEC ili chama kiwe na msimamo kuhusu BBI na kutathmini hatua zilizopigwa katika utekelezaji wa manifesto ya chama,” akasema Mbunge wa Soy, Bw Caleb Kositany, mwandani wa Naibu Rais.

Kauli yake iliungwa mkono na wabunge Brighton Yegon (Konoin), Didmus Barasa (Kimilili) na Oscar Sudi (Kapseret).

“Kulingana nami, Rais anaonekana amekihama chama tawala na kibarua kilichosalia kwetu ni kuendeleza chama hiki kwa sababu kiongozi wa chama anaelekea kustaafu,” akasema Bw Baraza.

Hata hivyo, mbunge wa Cherang’anyi, Bw Joshua Kutuny anapinga kauli ya wenzake akisema hakuna haja ya mikutano ya NEC au PG kwa sababu wale wanaohusika ndio wamekuwa wakimtusi na kumkejeli Rais hadharani.

Bw Kutuny anapendekeza kuwa chama kinafaa kubuni kamati ya kuwaadhibu wanaopinga ajenda za serikali.

You can share this post!

Yaibuka magavana walifuja pesa kufadhili BBI

Gavana apiga muuguzi kalamu kwa kuchelewa kufika kazini

adminleo