• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Ujanja wa Uhuru na Raila kuzima sauti zinazokosoa BBI

Ujanja wa Uhuru na Raila kuzima sauti zinazokosoa BBI

Na BENSON MATHEKA

Kwa miaka miwili sasa, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga wamekuwa wakipanga jinsi ya kubadilisha katiba kwa sababu ya kile wanachotaja kuwa kuunganisha Wakenya ili kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi.

Mchakato huu walioasisi kufuatia handisheki yao mnamo Machi 9 2018 ulianza kwa kupingwa na vigogo wengi wa siasa ambao walihisi kwamba ulikuwa wa kulinda maslahi ya viongozi hao wawili pekee.

Kulingana na Naibu Rais William Ruto, mchakato huo ulinuiwa kubuni nyadhifa za uongozi kwa wanasiasa wachache na haukuwa na lolote la kufaidi Mkenya wa kawaida.

Njama

Dkt Ruto alifaulu kushawishi baadhi ya wanasiasa hasa wabunge wa chama tawala cha Jubilee upande wake na kuzunguka kote nchini wakikosoa vikali mpango wa kubadilisha katiba. Kulingana nao, Mipango wa Maridhiano (BBI) ulikuwa njama ya Bw Odinga ya kuvuruga ajenda za serikali ya Jubilee.

Walilaumu baadhi ya watu wenye ushawishi kwa kupanga njama kumzuia Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Hata hivyo, Rais Kenyatta na Bw Odinga walisisitiza kuwa BBI haihusu siasa za urithi za 2022 bali nia yao ni kutatua shida zinazowakumba Wakenya kila baada ya miaka mitano wakati wa uchaguzi mkuu.

Kulingana nao walitaka kutia kikomo fujo zinazoacha nje ikiwa imegawanyika kila baada ya uchaguzi mkuu. Dkt Ruto na wandani wake waliendelea kumrushia lawama Bw Odinga huku wakiepuka kumtaja Rais Kenyatta moja kwa moja.

Mchakato huo ulisababisha migawanyiko mkubwa katika chama cha Jubilee na mirengo miwili ikazuka, mmoja unaomuunga Dkt Ruto (Tangatanga) na mwingine ukiunga Rais Kenyatta na handisheki yake na Bw Odinga ( Kieleweke).

Mwanzoni, Dkt Ruto alikuwa na imani kuwa angesambaratisha BBI kupitia bunge ambako wandani wake walikuwa waneshikilia nyadhifa za uongozi.

Kwenye mikutano waliyoandaa kote nchini hasa makanisani, walijigamba kwamba walikuwa na idadi kubwa ya wabunge na wakasisitiza kuwa juhudi zote za kurekebisha katiba zinapaswa kufanywa na bunge.

Dkt Ruto alikuwa amethibiti chama tawala cha Jubilee jambo lililompa nguvu za kupenya katika ngome za Rais Kenyatta katika eneo la Mlima Kenya kupinga BBI.

Alifaulu pia kupenya katika ngome za Bw Odinga eneo la pwani na magharibi ambako alijshindia wabunge kadhaa na kuendeleza upinzani dhidi ya BBI.

Mabadiliko

Hata hivyo, mbinu hii dhidi ya BBI ilizimwa wakati Rais Kenyatta alipofanya mabadiliko katika usimamizi wa chama na kuwaondoa wandani wa Dkt Ruto.

Naibu mwenyekiti wa chama hicho David Murathe ambaye alikuwa ametangaza kujiuzulu akisema hawezi kuketi katika kamati moja na Dkt Ruto alirudia majukumu yake akisema kiongozi wa chama Rais Kenyatta, hakukubali kujiuzulu kwake.

Washirika wa Dkt Ruto walipokonywa nyadhifa za uongozi bungeni na nafasi zao kupokezwa wandani wa Rais Kenyatta na Bw Odinga. Ili kumtoa pumzi Dkt Ruto na kuhakikisha ana idadi kubwa ya wabunge wanaomuunga mkono, Rais Kenyatta alitia mkataba wa ushirikiano na vyama vya Kanu, chama cha mashinani na Wiper.

Alikabidhi wabunge wa vyama hivi uongozi wa kamati za bunge zilizoshikiliwa na wandani wa Ruto.

Vuta ODM

Kwa kuwa tayari alikuwa amevuta chama cha ODM upande wake kupitia handisheki, Rais Kenyatta alifaulu kuzima tisho lolote la bunge kuzima BBI.

Hii ilimfanya Dkt Ruto kubadilisha mbinu na kubadilisha mrengo wa Tangatanga kuwa vuguvugu la kuinua maisha ya walalahoi lengo likiwa ni kuendeleza upinzani dhidi ya BBI.

Kupitia vuguvugu hilo la Hasla Nation, Dkt Ruto alijisawiri kuwa mtetezi wa wanyonge na kukosoa BBI kwa kupuuza maslahi ya Wakenya wa kawaida.

“Tutabadilisha majadala huu. Hatutaki mchakato ambao unapuuza maslahi ya mamilioni ya mahasla huku tukibadilisha katiba kutengea watu wachache nyadhifa za uongozi,” alinukuliwa akisema katika mikutano mingi aliyofanya nchini.

Kwa sababu ya kupinga BBI, Dkt Ruto alionekana kutengwa serikalini huku majukumu yake yakikabidhiwa waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i.

Baadhi ya mawaziri walianza kumdharau hadharani wakikosa kumtambua na kumuita karani wa Rais. Wandani wake waliokuwa msitari wa mbele kupinga BBI walianza kuandamwa na kutishwa kushtakiwa kwa makosa mbali.

Vigogo wa vyama vya kisiasa akiwemo Musalia Mudavadi wa Amani National Congress (ANC) na Moses Wetangula wa chama cha Ford Kenya pia walishawishiwa kuunga BBI ingawa awali walikuwa wakiipinga. Wadadisi wa siasa wanasema walibadilisha nia baada ya kugundua kuwa mchakato huo ni mradi wa serikali na ni vigumu kuuzima hata wakiupinga.

“Walifuatilia safari ya mchakato huo na kubaini ni mradi wa serikali ambao ni vigumu kushindana nayo. Kumbuka masaibu ya Wetangula ya kumbandua kama kiongozi wa chama cha Ford Kenya yalisemekana kutokana na upinzani wake kwa BBI,” asema mdadisi wa siasa Peter Koech.

Anasema kwamba Dkt Ruto alibaini kuwa ukiwa mradi wa serikali, hangefaulu kuupinga na ndio sababu anacheza karata kuhusu kura ya maamuzi asipoteze wafuasi aliokuwa amepata kwa kukosoa mchakato huo.

Wadadisi wa kisiasa wanasema ni wazi kuwa vinara wa mchakato huo wako na ajenda fiche na ndio sababu walipuuza utaratibu ufaao wa kubadilisha katiba na kuupatia kipaumbele wakati nchi inakabiliwa na changamoto nyingi.

You can share this post!

Watoto 88 wazaliwa Krismasi Eldoret

Shahbal aonekana kufaidika na siasa za kumrithi Joho