• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Kura ya Matungu kipimo cha umaarufu wa Mudavadi

Kura ya Matungu kipimo cha umaarufu wa Mudavadi

Na LEONARD ONYANGO

UCHAGUZI mdogo wa ubunge katika eneobunge la Matungu, Kaunti ya Kakamega, kitakuwa kipimo cha umaarufu wa kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi katika eneo la Magharibi.

Iwapo mwaniaji wa ANC Peter Oscar Nabulindo atabwagwa katika uchaguzi huo, wadadisi wa masuala ya siasa wanasema, litakuwa pigo kwa Bw Mudavadi na ishara kwamba amepoteza ushawishi wa kisiasa katika eneo la Magharibi.

Lakini ushindi wa Bw Nabulindo, utakuwa afueni kwa Bw Mudavadi ambaye kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2017 alitawazwa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli kuwa msemaji wa jamii ya Waluhya.

Hofu ya kupoteza kiti cha Matungu ilisababisha chama cha ANC kumpa Bw Nabulindo tiketi ya moja kwa moja kwa ajili ya uchaguzi mdogo utakaofanyika Machi 4, mwaka ujao.

Kiti hicho kiliachwa wazi kufuatia kifo cha Justus Muruga aliyechaguliwa kushikilia wadhifa huo 2017 kupitia chama cha ANC.Chama hicho kinachoongozwa na Bw Mudavadi kinahofia kuwa huenda kikapoteza kiti hicho kwa mwaniaji wa ODM au mgombeaji atakayeungwa mkono na Naibu wa Rais William Ruto.

Bw Odinga analenga kutumia uchaguzi huo mdogo kudhihirisha kuwa angali na ushawishi wa kisiasa katika eneo la Magharibi. Naye, Naibu wa Rais Ruto analenga kudhihirisha kuwa anakubalika katika maeneo ya Magharibi haswa baada ya mwaniaji wa kujitegemea Feisal Bader aliyekuwa akimuunga mkono kushinda katika uchaguzi mdogo wa Msambweni.

Mwendazake Muruga alikuwa mwandani wa Dkt Ruto na alikuwa nguzo muhimu wa Naibu wa Rais katika maeneo ya Magharibi.“Vyama vya kisiasa vitatumia fedha nyingi kufanya kampeni katika eneobunge la Matungu kwani Bw Mudavadi, Bw Odinga na Dkt Ruto wanataka kutumia uchaguzi huo mdogo kuonyeshana ubabe wa kisiasa,” anasema Bw Mark Bichachi, mdadisi wa masuala ya siasa.

Bw Nabulindo aliwania ubunge wa Matungu katika uchaguzi uliopita kupitia chama cha Ford Kenya na akaibuka nafasi ya pili baada ya kubwagwa na Murunga.

Chama cha ANC kinaamini kuwa Bw Nabulindo atashinda kwa sababu anaungwa mkono na ukoo wa Bashitsetse wa jamii ya Wawanga. Wanga ni moja ya makabila madogo ya jamii ya Waluhya.

Katika juhudi za kukwepa kugawanya kura, chama cha Ford Kenya tayari kimetangaza kuwa kitaunga mkono mwaniaji wa ANC.Kiongozi wa ANC Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula wamekuwa wakizungumza kwa sauti moja katika siku za hivi karibuni.

Wanasiasa waliokuwa wakimezea mate kiti hicho kupitia chama cha Ford-Kenya, wamekerwa na hatua ya Ford Kenya kuunga mkono mwaniaji wa ANC.

Aliyekuwa kiongozi wa vijana ngazi ya kitaifa wa Ford Kenya, Bw Bernard Wakoli, amegura chama hicho na kuwania kiti hicho kama mgombea wa kujitegemea.

Bw Wakoli ni miongoni mwa wawaniaji wanane wa kujitegemea ambao wametangaza nia ya kuwania kiti hicho.Mjane wa Murunga, Bi Christabel Murunga pia ameidhinishwa kuwania wadhifa huo.

Mwenyekiti wa Hazina ya Ustawi wa Eneobunge (NG-CDF) la Matungu, Bw Athman Wangara Khamisi, na meneja wa eneobunge hilo Bw Odanga Mutimba Pessa pia wameidhinishwa kuwania wadhifa huo kama wawaniaji wa kujitegemea.

Wawaniaji huru wengine watakaoshiriki uchaguzi huo mdogo ni Samuel Munyekenye, Wilberforce Chitechi Luttah, Notcus Borry Kevin na Stanslaus Kubende.

Vile vile, kutakuwepo Bw Charles Lutta Kasamani ambaye alikuwa akijiandaa kushiriki mchujo wa ANC lakini akagura baada ya uongozi wa chama kumpa tiketi ya moja kwa moja Bw Nabulindo.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imevitaka vyama kutatua mizozo inayohusiana na uteuzi kufikia Januari 4, 2021.Chama cha ANC sasa kimemtaka Bw Odinga kutosimamisha mwaniaji katika uchaguzi huo mdogo kama ‘shukrani’ kwa Bw Mudavadi.

Dkt Ruto huenda akaunga mkono mmoja wa wawaniaji wa kujitegemea.Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa ambaye ni mwandani wa Naibu wa Rais aliambia ukumbi huu Dkt Ruto ataunga mkono mwaniaji wa kujitegemea aliye na umaarufu.

Kupitia kwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, chama cha ANC kilisema kuwa Bw Odinga atajidhihirisha kama mtu asiyekuwa na shukrani iwapo ODM kitashiriki katika uchaguzi huo mdogo.

“Bw Mudavadi alisitisha azma yake ya kutaka kuwania urais 2017 na kuunga mkono Bw Odinga. Kiongozi wa ODM hana budi kuonyesha shukrani kwa kukosa kusimamisha mwaniaji katika uchaguzi mdogo wa Matungu,” akasema Bw Malala.

You can share this post!

UGAVANA NAIROBI: Margaret Wanjiru alivyogeuka mwiba kwa...

Masaibu ya Gor Mahia kwenye CAF Champions League