• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
LEONARD ONYANGO: Uchaguzi mdogo Nairobi ndio mtihani halisi kwa BBI na Ruto

LEONARD ONYANGO: Uchaguzi mdogo Nairobi ndio mtihani halisi kwa BBI na Ruto

Na LEONARD ONYANGO

TANGU mwaniaji wa kujitegemea Feisal Bader – aliyekuwa akiungwa mkono na Naibu wa Rais William Ruto – kushinda kiti cha ubunge katika uchaguzi mdogo wa Msambweni, kumekuwa na mjadala mkali kuhusu hatima ya mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Baadhi ya wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa ushindi wa Bader ulikuwa ishara kwamba chama cha ODM kilichokuwa kimesimamisha Bw Omar Boga, kimeishiwa na umaarufu katika maeneo ya Pwani.

Nao wandani wa Naibu wa Rais Ruto, wanadai kuwa matokeo ya uchaguzi mdogo yalikuwa kidokezo kwamba Wakenya hawana haja na BBI. Hii ilikuwa baada ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kueleza wakazi wa Msambweni kuwa kushindwa kwa Bw Boga kungekuwa pigo kwa BBI.

Lakini wanasiasa wa ODM wanajitetea kwa kusema kuwa huenda wakazi wa Msambweni walichagua Bader kwa sababu ni mpwa na mwandani wa aliyekuwa mbunge wa eneobunge hilo Suleiman Dori aliyefariki Machi mwaka huu.

Lakini uchaguzi mdogo wa ugavana wa Kaunti ya Nairobi ndicho kitakuwa kipimo halisi cha BBI.Iwapo mwaniaji anayeungwa mkono na mrengo wa handisheki atabwagwa katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Februari 18, mwaka ujao, basi huo ndio utakuwa mwisho wa BBI. Hii ni kwa sababu Nairobi ina wapigakura wanaotoka katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Kaunti ya Nairobi, vilevile, ina idadi kubwa ya wapigakura hivyo ni rahisi kutumia matokeo kutabiri mwelekeo wa mawimbi ya kisiasa nchini.

Japo Dkt Ruto hajatangaza mwaniaji atakayemuunga mkono, kuna dalili kwamba huenda akampigia debe aliyekuwa mbunge wa Starehe, Bi Margaret Wanjiru.

Lakini ikiwa chama cha Jubilee kitakuwa na mwaniaji wa ugavana, Dkt Ruto atajipata kwenye njiapanda. Itabidi aunge mkono mwaniaji wa Jubilee na kuachana na wawaniaji wa kujitegemea.

Endapo Naibu wa Rais ataunga mkono mwaniaji wa kujitegemea na kuacha atakayesimamishwa na Jubilee, mahasimu wake wa kisiasa watatumia fursa hiyo kumshinikiza kujiuzulu au kuanzisha harakati za kumtimua.

Lakini iwapo Dkt Ruto ataunga mwaniaji tofauti na chama cha Jubilee mgombea wake ashinde, hiyo itakuwa ishara kwamba njia yake ya kuelekea Ikulu baada ya uchaguzi mkuu wa 2022 imenyooka.

Mwaniaji atakayeungwa mkono na Dkt Ruto akibwagwa basi itakuwa na athari kubwa katika safari yake ya kuelekea Ikulu.

You can share this post!

Mbunge wa zamani wa Kaloleni afariki

Lalama zazuka baada ya polisi katili kutetewa