Waislamu waungana kupinga BBI

Na BENSON MATHEKA

VIONGOZI wa dini ya Kiislamu wamesisitiza kauli yao ya awali kuwa mchakato wa kubadilisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) utagawanya Wakenya hata zaidi na hivyo unafaa kusitishwa mara moja.

Wakizungumza jijini Nairobi, viongozi wa Baraza la Waislamu Kenya (Supkem), Baraza la Wahubiri wa Kiislamu (CIPK), Jukwaa la Kitaifa la viongozi wa Kiislamu (NAMLEF) na Muungano wa Vijana wa Kiislamu walimhimiza Rais Kenyatta kuweka breki kura ya maamuzi na badala yake kushughulikia masuala ya uchumi, janga la corona na ukiukaji wa haki za binadamu.

“Tunafaa kutafuta sababu za kutuunganisha kuliko za kututenganisha. Tunafaa kutafuta hekima ya kutambua tunakoelekea kupitia njia hatari ya mgawanyiko. Njia hii ambayo mara nyingi hufuatwa na wanasiasa husababisha chuki za kikabila, kidini na kitabaka,” viongozi hao walionya kwenye taarifa ya pamoja.

“Tunamuomba Rais Kenyatta kutambua haja ya kusimamisha BBI kwa kuwa inagawanya Wakenya. Tunamuomba kama nebo ya umoja wa taifa, kukumbatia mjadala wa kitaifa ili kujenga uwiano,” walisema.

Walisema taifa linakabiliwa na changamoto za corona, uchumi kuporomoka, utaifa kudorora, haki za binadamu kukiukwa na kupuuzwa kwa utawala wa sheria ikiwa ni pamoja na maafisa wa serikali kupuuza maagizo ya korti.

Waliotia saini taarifa hiyo ni Sheikh Hassan Ole Naado wa Supkem, Sheikh Abdallah Ateka wa CIPK, Sheikh Abdullah Abdi wa Namlef na Abdulhamid Sakar kwa niaba ya vijana.

Viongozi hao walisema licha ya BBI kusemekana kuwa ya kukuza utaifa, imekuwa ajenda ambayo imegawanya Wakenya zaidi mwaka huu.

“Tumeona kila wakati viongozi wa kisiasa wanapopatiwa nafasi hadharani, wanaitumia kuonyesha tofauti zetu badala ya kuitumia kutuunganisha. Wakenya wanashangaa kuwa licha ya umasikini kuongezeka na hali isiyotabirika siku zijazo, viongozi wa kisiasa wanaamua kupatia kipaumbele jumbe za kugawanya, chuki na uhasama,” walisema.

Waliomba serikali kufikiria upya kurejeshwa kwa viwango vya kodi wakisema hatua hiyo haikufaa kuchukuliwa bila kuhakikishia biashara zimefufuka na uchumi kuimarika.

Walisema taifa limeathiriwa vibaya na corona na wakakashifu waliotumia janga hilo kupora pesa za umma.“Kwamba watu hao, baadhi yao wanaosemekana kuwa viongozi katika serikali na sekta ya kibinafsi wangali huru wakifurahia matunda ya ufisadi ni mtihani kwa tume na idara zinazohusika na ufisadi na mashtaka,” walisema.

Habari zinazohusiana na hii

Acha katambe

Kwa nini tunapinga BBI

Hisia mseto kuhusu BBI