Chama cha ‘wilbaro’ chapata mwanga wa kusajiliwa

Na LEONARD ONYANGO

MSAJILI wa Vyama vya Kisiasa ameruhusu chama cha Party for Development Reform (PDR) kutumia nembo ya ‘wilibaro’ ambayo imekuwa ikitumiwa na Naibu wa Rais William Ruto kushawishi walala hoi.

Kupitia notisi iliyochapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali Jumatatu, chama cha PDR pia kimebadilisha jina na kauli mbiu yake.Iwapo hakutakuwa na pingamizi baada ya siku saba, chama cha PDR sasa kitajulikana kama United Democratic Alliance (UDA) na kaulimbiu yake itabadilika kuwa ‘Kazi ni Kazi’.

Kwa sasa chama hicho kinatumia kaulimbiu ya ‘Mabadiliko na Ustawi’.Dkt Ruto amekuwa na kaulimbiu ya ‘Mboka ni Mboka’ ambayo ni lugha ya Sheng’ inayomanisha kazi ni kazi.

Jana, Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Nderitu aliambia Taifa Leo kuwa haijulikani ikiwa wamiliki wa chama cha PDR wanaegemea mrengo wa Dkt Ruto au upande wa handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Chama cha PDR kilisajiliwa mnamo 2016, kwa mujibu wa Bi Nderitu.Novemba 12, gazeti la Taifa Leo liliripoti kuwa afisa ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa ilikuwa imepokea maombi kadhaa kutoka kwa watu waliotaka kutumia wilibaro kama nembo ya vyama vyao.

Ni kawaida kwa watu kukimbilia kutuma maombi kusajili jina au neno ambalo ni maarufu kwenye ulingo wa kisiasa. Kwa mfano, baada ya upande wa ‘La’ uliowakilishwa na chungwa kushinda kura ya maamuzi ambapo Wakenya walikataa rasimu ya katiba mnamo 2005, wakili Mugambi Imanyara alisajili chama cha chungwa (ODM).

Baadaye alikikabidhi kwa kiongozi wa ODM Raila Odinga wakati uchaguzi mkuu wa 2007 ulipokaribia na Bw Imanyara akawa katibu wa masuala ya sheria ya chama hicho, wadhifa alioshikilia hadi 2011.

Wilibaro zimekuwa zikihusishwa na Naibu wa Rais William Ruto hivi karibuni.Wapinzani wake, wakiongozwa na Bw Odinga, wamekuwa wakishutumu Dkt Ruto kwa ‘kuwahadaa vijana kwa kuwapa wilibaro ambayo imepitwa na wakati’.

Lakini Naibu wa Rais anashikilia kuwa wilibaro ni muhimu kwa wafanyabiashara wadogo wasiomudu gharama ya kukodisha maeneo ya kuuzia bidhaa zao.Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa ilitupilia mbali ombi la kutaka kusajili Mpango wa Maridhiano (BBI) kuwa chama cha kisiasa.

Watu wasiojulikana walijaribu kusajili BBI baada ya baadhi ya wanasiasa kupendekeza kiwe chama kitakachojumuisha wanasiasa wanaounga mwafaka baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Miezi mitatu iliyopita Bi Nderitu, alikataa maombi ya kutaka kusajili Jubilee Asili na ‘Hustler’ kuwa vyama vya kisiasa huku akisema kuwa majina hayo yanakiuka sheria.

Maombi ya kutaka kusajili chama cha Jubilee Asili yalimiminika baada ya Naibu wa Rais Ruto mnamo Juni, mwaka huu, kuzindua afisi mbadala yenye jina Jubilee Asili Centre katika mtaa wa Kilimani jijini Nairobi na kuzua tetesi kuwa huenda alitaka kuunda chama kipya.

Lakini mmiliki wa jumba hilo tayari ametimua wanasiasa wa Tangatanga kutoka kwenye jumba hilo huku akisema kuwa anataka kulitumia kwa matumizi mengineyo.

Habari zinazohusiana na hii

Acha katambe

Kwa nini tunapinga BBI

Hisia mseto kuhusu BBI