• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
MARY WANGARI: Tuwe na matumaini 2021 itakuwa yenye heri njema

MARY WANGARI: Tuwe na matumaini 2021 itakuwa yenye heri njema

Na MARY WANGARI

IWAPO kuna mwaka ambao umesheheni mitihani tele kwa Wakenya na binadamu wote kwa jumla duniani, basi ni 2020.

Mwaka huu utakumbukwa kama kipindi mojawapo katika historia kilichovuruga na kubadilisha kabisa hali ya kawaida ya maisha ya binadamu na kuanzisha enzi mpya.

Ni katika 2020 ambapo tulishuhudia mifumo ya kiuchumi nchini na kimataifa ikitikiswa na kusambaratishwa kabisa pasipo kubagua hadhi ya taifa katika ramani ya dunia.

Licha ya maendeleo kiteknolojia, kiutandawazi ikiwemo silaha hatari za kivita kama vile nuklia, mifumo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi duniani ilisambaratishwa na kuwaacha viongozi wa ulimwengu wakijikuna vichwa wasijue la kufanya.

Yote haya ni kutokana na janga la virusi hatari vya corona ambavyo licha ya chanjo dhidi yake kupatikana tunapoelekea kuuaga mwaka huu, vimeendelea kuwakosesha usingizi wanasayansi na matabibu ulimwenguni kote.

Taharuki, simanzi na maafa yasiyoelezeka ni baadhi tu ya mashaka ambayo yamekumba binadamu na kufanya wengi kushukuru kwa kupata fursa ya kuwa hai angalau kwa siku moja nyingine tu.

Kando na athari hasi, Covid-19 pia imekuwa na athari chanya na mafunzo tele muhimu.Janga hili kwa mfano, limewaacha binadamu bila hiari ila kutilia maanani masuala muhimu ya kibinadamu ambayo yamepuuzwa kwa muda mrefu kutokana na shinikizo za kila uchao za kimaisha.

Mwaka wa 2020 utaingia kwenye vitabu vya kihistoria kama kipindi ambapo watoto na wazazi walipata nafasi ya kuwa pamoja kwa muda wa kutosha baada ya taasisi za elimu kote duniani kufungwa.

Isitoshe, hali ya kusitishwa kwa shughuli za kikazi, usafiri na marufuku tofauti duniani, iliwezesha familia, jamaa na walio katika mahusiano kuwa na muda wa kutosha pamoja.

Hali hiyo, hata hivyo, ilimshurutisha binadamu kukabiliana na uhalisia mchungu kwamba kwa muda mrefu, wamekuwa wakikimbizana na mambo mengi na kupuuza masuala nyeti.

Mafarakano baina ya baadhi ya wanandoa ikiwemo visa vingi vya talaka na utengano vilivyoripotiwa ni baadhi ya ukweli wa kutamausha uliojitokeza.Aidha, utepetevu katika malezi ya watoto ulikuwa dhahiri huku baadhi ya wazazi wakigutuka kwamba hawawafahamu watoto wao.

Hata hivyo, ni katika 2020 vilevile ambapo ukakamavu, ari ya binadamu kuendelea kuishi licha ya mitihani sugu na kumudu mabadiliko, ulipowekwa kwenye vipimo na kupasi kwa namna ya kuvutia.

Lilikuwa ni jambo la kuonea fahari si haba, kuona baadhi ya mataifa barani Afrika wakichangia kukabiliana na Covid-19 kupitia uvumbuzi anuai badala ya kusubiri tu msaada kutoka kwa mataifa makuu.

Tunapoingia 2021, kwa neema na rehema za Mwenyezi Mungu, tunapaswa kuwa na matumaini kwamba hali itatengenea na kuwa na heri njema.

[email protected]

You can share this post!

Ugaidi Lamu ulipungua 2020

WHO yatoa tahadhari ya corona kuleta kisonono sugu