• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 5:55 AM
BENSON MATHEKA: Polisi wakomeshe dhuluma kwa raia

BENSON MATHEKA: Polisi wakomeshe dhuluma kwa raia

Na BENSON MATHEKA

KUONGEZEKA kwa visa vya ukatili ambao polisi wanatendea raia wasio na hatia nchini kunaweza kuathiri uchumi. Maafisa hao wamekuwa wakitajwa na kuhusishwa na kila aina ya uhalifu na maovu wanayopaswa kupigana nayo kwa kutumia sheria.

Wanajigamba kuwa wao ndio sheria na ikizingatiwa kwamba wamekuwa wakiepuka adhabu huku wakiendelea kuwadhulumu raia, huenda Wakenya wakaamini kweli sheria haithibiti maafisa hao.

Kauli mbiu ya idara ya polisi ya utumishi kwa wote imebaki kuwa utumishi kwa walio nacho. Maafisa wa polisi wamekuwa wakiwahudumia wanaoweza kuwapa hongo pekee na kuwapuuza wale wasio na uwezo wa kufanya hivyo.

Hii imefanya wengi kuchukulia kuwa polisi wanahudumia tabaka fulani la Wakenya. Kwa miaka mingi, polisi wa Kenya wamekuwa wakiorodheshwa miongoni mwa walio fisadi na katili zaidi ulimwenguni. W

ametumiwa na watu wenye ushawishi kudhulumu raia, wamehusishwa na matumizi ya nguvu kupita kiasi wakitekeleza kazi yao kwa maagizo ya watu wanaolenga kuhangaisha wengine na hii inaweza kuwatia hofu wawekezaji.

Kampuni za kimataifa na za watu binafsi huchagua kuwekeza katika mazingira salama kwa biashara na watumishi wake na sio katika nchi ambayo wanaopaswa kuwahakikishia usalama ndio wanaohusika na uhalifu.

Hali hii inazidishwa na hatua ya wakuu wa polisi kuwatetea wanaotekeleza uhalifu jambo linalowapa maafisa hao nguvu za kuendeleza vitendo vyao vya dhuluma kwa raia.

Katika kisa cha hivi punde, Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Nzioki Mutyambai na Mwenyekiti wa Huduma ya Polisi Eliud Kinuthia waliwatetea maafisa watatu wa polisi walionaswa kwenye video wakimshambulia mfanyabiashara wa Naivasha eneo la Nakuru ambaye hakuwa na silaha.

Wanachosahau wakuu hao wa polisi ni kwamba teknolojia imeimarika ambapo matukio yanaweza kunaswa na kuanikwa mitandaoni ulimwengu ushuhudie na kufanya uamuzi.

Wawekezaji huwa wanatumia mitandao kupata habari kuhusu nchi wanazopania kuwekeza. Kuwatetea na kuwalinda maafisa katili ambao vitendo vyao vimeanikwa wazi kunaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi.

Inashangaza wakuu wa polisi wanaweza kuwa na ujasiri wa kulaumu raia kwa kushambulia maafisa wa usalama wanaotenda maovu wakivalia sare za kazi wanapofanya kazi yao.

Wakuu hao wanafaa kutumia ujasiri huo kuwaadhibu vikali maafisa wanaofyatulia risasi na kuwaua watoto, watu walio na ulemavu na kuitisha hongo kutoka kwa wanaoenda kuripoti visa vya ubakaji na unajisi vituoni. Ni kweli ni makosa makubwa kwa raia kushambulia maafisa wa polisi na kila mmoja anafaa kuepuka tabia hiyo.

Hilo halikubaliki kamwe. Hata hivyo, maafisa hao wanafaa kuepuka kudhulumu raia ili wakome kuwachukulia kuwa maadui wao. Maafisa hao hufunzwa misingi ya kuheshimu haki za binadamu na kukataa maagizo yaliyo kinyume cha sheria lakini vitendo vyao vinaenda kinyume na mafunzo hayo.

Kwa nchi kupata ufanisi wa kiuchumi, utawala wa sheria, viwango vya juu vya usalama unaotokana na utaalamu wa maafisa wa polisi zinafaa kudhihirika.

Maafisa wa usalama wanapokuwa msitari wa mbele kwa ufisadi, ni vigumu kuangamiza uovu huo, wanapokuwa msitari wa mbele kuvunja sheria, wananchi huchukua sheria mikononi na kufanya nchi kuvurugika na kukosa mazingira ya uwekezaji

You can share this post!

Hakuna wa kunizuia kuwania ugavana Nairobi – Baba Yao

Matiang’i apotosha kuhusu uhalifu