• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
Usiwatambue Wapemba kwa vilemba pekee, wana sifa nyingine tumbi nzima

Usiwatambue Wapemba kwa vilemba pekee, wana sifa nyingine tumbi nzima

Na HAWA ALI

PEMBA ni kisiwa kilichoko pembezoni mwa mwambao wa pwani ya Afrika Mashariki; kwenye bahari ya Hindi. Kisiwa hiki ni cha takribani kilomita hamsini mraba.

Kinapatikana Kaskazini Mashariki ya kisiwa cha Unguja na kilomita hamsini Mashariki ya pwani ya Tanganyika. Kisiwa hiki kina historia ndefu inayohusiana na ukaaji binadamu. Kazi za asili za wakazi wa kisiwa hiki ni ukulima mdogo.

Mazao mashuhuri ya chakula yanayozalishwa kisiwani hapa ni mpunga, mihogo, maharagwe chooko na kunde. Vilevile, wakazi hujishughulisha na shughuli za uvuvi.

Mji mkuu wa kisiwa cha Pemba ni Chake uliojitenga juu ya kilima.Kwa asili Wapemba ni watu wenye asili ya uzawa wa kisiwa cha Pemba. Lugha wanayozungumza ni Kiswahili.

Lahaja inayozungumzwa na Wapemba inaitwa Kipemba. Ni moja ya lahaja za Kiswahili kinachozungumzwa kisiwani Pemba pekee.Utamaduni wa Wapemba ni ule wa Mswahili wenye kuhimiliwa katika mila na desturi halisi za Waswahili.

Mila za wenyeji hutokana na utamaduni ambao wanaamini huwaletea upendo wa kuishi kijamaa, kimitaa au kivijiji. Mathan kula pamoja, kuabudu pamoja na kusaidiana katika malezi, uuguzi, ndoa, tiba wakati wa misiba na kadhalika.

Mavazi

Kimavazi, Wapemba wana desturi ya mavazi changamano, ambayo ni pamoja na uvaaji wa mashati maalum, shuka, suruali, kanzu, kofia za viua au mfuto, viatu vya miti, mipira au ngozi kwa wanaume.

Mavazi ya wanawake ni pamoja na kanzu, shumizi, buibui, kanga, kaniki, mitandio na viatu vya ngozi. Wanawake wa Kipemba zaidi ya mavazi hayo wana mazoea ya kujipamba kwa vito vya dhahabu, fedha au kareti kama bangili, vidani, vipini, pete na herini.

Aidha, wao hutengeneza vikuba na mapambo mengine kwa kutumia maua yanayonukia kama mkadi, asumini, viluwa au mawaridi.

Wanawake hawa hupenda kujipaka hina na podari, rangi za midomo, mafuta mazuri ya haliudi, tarabizuna, miski pamoja na kujifukiza udi wa mawaridi pale wanapokuwa nyumbani, wanapokwenda harusini, safari ya matembezi au hata kazini.

You can share this post!

Kenya yapitisha marekebisho ya Sheria ya Pufya

Unyama magaidi wakilipua ambulensi ya mjamzito