Visa vya corona vyendelea kupungua

Na CHARLES WASONGA

KENYA Jumatano iliendelea kuandikisha kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya virusi vya corona baada ya watu 112 wapya kupatikana na virusi hivyo.

Hii ni baada ya sampuli kutoka kwa watu 3,327 kupimwa ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita, hivyo kiwakilisha kiwango cha maambukizi cha asilimia 3.2

Kulingana na taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe visa hivyo vipya vya maambukizi vimefikisha 96,251 idadi jumla ya maambukizi tangu kisa cha kwanza kilipogunduliwa mnamo Machi 13, 2020.

Bw Kagwe pia alitangaza kuwa ni watu wawili pekee waliothibitishwa kufariki Jumatano, kutokana na ugonjwa wa Covid-19, na hivyo kufikisha idadi jumla ya wagonjwa waliofariki kuwa 1,667.

Hii ni tofauti kabisa na hali ilivyokuwa katika mwezi wa Novemba ambapo wagonjwa 12 kwa wastani walikuwa wakifariki kutokana na homa hiyo hatari.

Bw Kagwe pia alitangaza kuwa wagonjwa 816 walipona kutokana na Covid-19 ndani ya muda wa saa 24 zilizopita na hivyo kufikisha idadi jumla ya waliopona kuwa 78,475.

“Miongoni mwo wagonjwa 798 walikuwa wakihudumiwa nyumbani ilhali 18 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini,” akasema.

Bw Kagwe pia alitangaza kuwa jumla ya wagonjwa 667 wa corona wakati huu wamelazw katika hospitali mbali nchini ilhali 3, 214 wanauguzwa nyumbani.

“Na wagonjwa 30 wako katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU), huku wengine 16 wakisaidiwa kupumua kwa mitambo maalum. Wagonjwa wengine 23 wanaongezwa hewa na oksijeni.

Kuhusiana na visa vipya vya maambukizi, Nairobi inaongoza kwa kuandikisha visa vipya 53, Mombasa (23) huku kaunti za Kakamega, Bungoma na  Kilifi zikiandikisha visa saba kila moja.

Nazo kaunti za Kajiado, Lamu na  Busia  ziliripoti visa viwili kila moja huku Nyeri, Siaya, Kwale, Machakos, Nakuru, Kiambu na Uasin Gishu zikinakili kisa kimoja cha maambuki kila moja.

Habari zinazohusiana na hii