• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 7:55 AM
Olunga kulenga juu zaidi baada ya makali yake ugani kutambuliwa na FIFA

Olunga kulenga juu zaidi baada ya makali yake ugani kutambuliwa na FIFA

Na CHRIS ADUNGO

MCHEZAJI Michael Olunga ameapa kulenga juu zaidi baada ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kumtia katika orodha ya wanasoka watano wa haiba kubwa ambao hawajulikana sana licha ya kuwika sana katika kampeni za mwaka wa 2020.

“Japo nimepokea ofa nyingi za kujiunga na vikosi mbalimbali vya bara Ulaya, lengo langu ni kusalia nchini Japan kwa matumaini ya kuendelea kufungiwa Kashiwa mabao mengi zaidi. Hata hivyo, wakala wangu atakuwa huru kutathmini hali ilivyo kabla ya kushauriana nami kuhusu maamuzi mengine muhimu kitaaluma,” akaongeza Olunga.

Olunga aliwahi kufichua ukubwa wa kiu ya kuingia katika sajili rasmi ya Arsenal ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) chini ya kocha wa zamani wa kikosi hicho, Arsene Wenger.

Nyota huyo wa zamani wa Gor Mahia alijivunia msimu wa kuridhisha katika Ligi Kuu ya Japan (J1 League) na akatawazwa Mchezaji Bora na Mfungaji Bora muhula huu baada ya kucheka na nyavu mara 28 kutokana na mechi 32.

Wanasoka wengine waliotambuliwa kwa pamoja na Olunga ni Marcel Hernandez wa Costa Rica, Kasper Junker wa Denmark. Ramiro Rocca wa Argentina na Rauno Sappinen wa Estonia.

Makali ya Olunga mbele ya malango ya wapinzani yalisaidia waajiri wake Kashiwa Reysol kukamilisha kampeni za msimu huu katika nafasi ya saba jedwalini licha ya kwamba walipandishwa ngazi mwishoni mwa muhula uliopita ulioshuhudia sogora huyo wa zamani wa Gor Mahia akifunga mabao 27.

Japo Olunga, 26, amewahi pia kuchezea nchini Uswidi, Uhispania na China, wepesi wake wa kufunga mabao umejitokeza katika kipindi cha misimu miwili iliyopita nchini Japan.

“Mafanikio yangu ulingoni ni zao la imani na bidii. Sikuwahi kutamauka hata nilipojikuta nikikabiliwa na changamoto tele. Natambua pia ukubwa wa mchango wa wanasoka wenzangu ambao waliniundia pasi nyingi zilizozalisha idadi kubwa ya mabao niliyofunga,” akasema Olunga katika mahojiano yake na Fifa.com.

Kati ya rekodi nyinginezo zinazojivuniwa na Olunga katika ulingo wa soka ni kuwahi kuwa sogora wa kwanza kufungia FC Girona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) jumla ya mabao matatu katika mechi moja ligini.

Mchezaji huyo wa zamani wa Liberty Sports Academy, Tusker FC na Thika United aliwahi pia kufungia Kashiwa jumla ya mabao manane katika ushindi wa 13-1 uliosajiliwa na kikosi hicho dhidi ya Kyoto Sanga katika Ligi ya Daraja la Pili mnamo 2019.

Kabla ya kujiunga na Girona kwa mkopo kutoka Guizhou Zhicheng ya China, Olunga aliwahi pia kusakata soka ya kulipwa kambini mwa Djurgardens IF ya Uswidi mnamo 2016.

Nyota huyo amekuwa tegemeo kubwa la timu ya taifa ya Harambee Stars na mabao yake dhidi ya Ghana na Ethiopia yalisaidia Kenya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo 2019 nchini Misri. Olunga alifungia Stars mabao matatu kwenye fainali hizo zilizowashuhudia wakibanduliwa mapema kwenye hatua ya makundi.

You can share this post!

AK yatoa ratiba kali ya Mbio za Nyika kwa maafisa wa...

Cavani kuendelea kusakatia Man United hata baada ya msimu...