• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:20 AM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Husuda ni donda linalotoneshwa na neema, fanaka za wanadamu

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Husuda ni donda linalotoneshwa na neema, fanaka za wanadamu

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mungu, Muumba wa mbingu na nchi.

Swala na salamu zimwendee Mtume Muhammad, SAW, maswahaba wake na watangu wema hadi Siku ya Kiyaamah.

Hasadi ni ugonjwa mbaya sana katika moyo wa mwanadamu. Husuda imeainishwa kama ni donda la moyo. Neema au mafanikio ya mtu hulitonesha donda hili na kumtia maumivu na machungu hasidi. Donda hilo huvuja damu na kulowesha moyo wote.

Mtume Alayhi Salaam ameifananisha husuda na moto. Mithili ya moto unavyoteketeza kuni ndivyo husuda inavyounguza amali za mtu. Kubwa zaidi ni aya maalum ya Qur’an ambayo inatutaka tujikinge kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya hasidi anapohusudu.

Mwanazuoni mmoja ameielezea husuda kwa maana mbili; mosi, ni moyo usiotaka mwingine apate, pili, ni moyo wa kumtakia mabaya mwingine kuwa neema aliyoipata iharibike au imtoke. Kwa kuitolea mifano zaidi husuda ni kwamba mtu mwenye moyo wa husuda huwa na mawili; ama apate yeye, au wakose watu wote.

Kama ni neema, moyo wake hufurahi mno unapoipata neema hiyo, na wakati huo huo haupendi wengine waipate. Lakini unapoikosa neema, moyo huo wa hasidi husononeka, husongeka na hukosa raha.

Hasidi akikosa yeye, basi hutamani na wengine wakose. Huwa tayari kufanya kila hila kuhakikisha kuwa mtu fulani hapati neema fulani. Na mtu huyo akipata, yeye, kwanza, hujiuliza kaipataje? Atadadisi hata kwa wengine kujua mtu huyo kapata-pataje na kapata wapi hiyo neema?

Kama atapata njia basi anaweza kujaribu kutia fitna ya kuhujumu neema hiyo ili apoze machungu ya donda la husuda moyoni mwake. Husuda ni ugonjwa ndani ya moyo, lakini athari zake zinaweza kudhihirika hata katika haiba ya nje ya kiwiliwili cha mtu. Mtu anaweza kukonda na kupoteza siha yake kwa husuda dhidi ya neema ya fulani.

Kinachomkondesha ni kwa nini fulani kapata, mimi sikupata? Kwa nini fulani anacho, mimi sina? Wakati mwingine, anaweza hata kusema maneno ya kuashiria husuda yake. Mathalani, mwenziwe anaweza kujenga nyumba nzuri, yeye badala ya kupongeza, husuda yake humfanya aseme, Ah! Mnajenga mijumba ya nini, dunia ni ya kupita tu hii!

Au anaweza kukebehi, hii nayo nyumba bwana! Si kwamba ana dhati moyoni kwa hayo anayoyasema, bali anajaribu kuufariji moyo wake unaowaka moto wa husuda. Ukithubutu kufanya kosa la kumfanya hasidi huyu akushauri katika mpango wako, anaweza kukuvurugia!

Kwa mfano, unataka kununua gari, sasa unaomba ushauri kwake, anaweza kukukatisha tamaa kwa kukwambia gari ya nini! au gari hasara! Na kama utanunua, husuda yake itampelekea kusema,

Si kwamba ana dhati na hicho anachokisema, bali moyo unamuuma. Watu wenye ugonjwa wa husuda huweza hata kumpumbaza mtu asifanye jambo fulani. Kama ni mtu wa dini, watamzubaisha kuwa asinunue gari wala asijenge nyumba, eti vitu hivyo ni vya kudunia tu, sisi tushughulikie Akhera tu.

Si kwamba wana dhati na hicho wanachokisema bali husuda kuwa fulani akifanya jambo fulani, atapata na kuwashinda wao.

Mtu akijiweka jirani zaidi na Mwenyezi Mungu kwa ibada nzito za usiku na mchana, na akijiepusha na maovu makubwa na madogo, hupata ulinzi wa Mola wake dhidi ya hasidi. Kadri anavyoisoma Qur’an na kusoma Hadith za Mtume, hupata tamiizi, ibra na uwezo mkubwa wa kujua undani wa wanadamu.

Mtu huyu anapojiwa na hasidi, anakuwa kama daktari wa magonjwa ya moyo hospitalini. Mgonjwa akisema, tayari yeye anajua huu ni ugonjwa gani wa moyo. Hasidi anapotamka tu jambo juu ya neema fulani, mtu mcha Mungu hung’amua, kwa nini huyu anasema hivi. Hatamjibu palepale, lakini moyoni na akilini mwake atajua afanye nini kumshinda hasidi huyo.

Si katika neema za mali tu, bali hata mambo mengine kama vile uchumba huweza kuvurugika kwa sababu ya mahasidi. Wakisikia tu binti fulani anataka kuolewa, basi itaundwa kamati maalum ya ufundi kuvuruga mpango mzima wa ndoa. Watatumiwa watu wanaokubalika upande wa mume ili ujumbe wa mahasidi ufike na kuzingatiwa.

Sio siri mipango mingi ya ndoa mitaani imesambaratishwa na mahasidi ambao hucheza karata zote. Wataanza kumshawishi mwanamke kuwa mume yule hafai, si riziki, ana ukimwi, akishaua wanawake wengi ili binti atimize wanachokitaka kwa ile husuda yao!

Asipowaelewa, wanatuma watu upande wa mume, wakaseme kuwa yule binti ni kahaba! hana kizazi! Kishagonga yule na ikitokea kuwa ndoa imefanyika licha ya vitimbi vyote hivyo, hawakati tamaa, bali watahakikisha inavunjika. Hata zinaposalia dakika za mwisho kabisa za ndoa kufungwa, mahasidi hawakati tamaa.

You can share this post!

Chiloba sasa apata kazi serikalini baada ya kutimuliwa na...

Uhuru awatakia Wakenya heri njema 2021