KAMAU: Ukosefu wa falsafa bora ulivyovuruga siasa zetu

Na WANDERI KAMAU

MSINGI thabiti wa kisiasa ni mojawapo ya nguzo kuu katika ustawi wa jamii ama taifa lolote lile duniani.

Hilo hujenga mazingira yafaayo kwa masuala mengine muhimu katika jamii husika kuendelea na kupanuka bila vikwazo vyovyote.

Hata hivyo, mkosi huiandama jamii ikiwa itakosa kukuza na kudumisha mfumo thabiti wa kisiasa, unaotambulika virahisi na kuzingatiwa na wanajamii wake.

Duniani kote, kuna mifano mingi ya nchi ambazo zimestawi sana kisiasa, kiuchumi na kitamaduni kwa kukuza mifumo thabiti ya kisiasa.

Kando na kutambulika na wanajamii, mifumo hiyo pia hujenga mazingira ya uwajibikaji kwa taasisi zote zilizo kwenye jamii husika.

Hiyo ndiyo sababu kuu ambapo ni vigumu kwa jamii zinazozingatia mifumo hiyo kukumbwa na maovu kama ufisadi ama kutowajibika kwa maafisa wakuu wa serikali.

Je, Kenya i wapi?

Inasikitisha sana kuwa Kenya ni miongoni mwa jamii ambazo zimeshindwa kabisa kubuni mfumo maalum wa kisiasa, ambao unatoa utambulisho fulani kuhusu sera na utaratibu wa uongozi wake.

Ingawa ni taifa linalodai kuzingatia mfumo wa kidemokrasia katika utawala wake, bado halijajenga utamaduni maalum kuhusu mfumo wake wa uongozi.

Hili huwa linadhihirika kila uchaguzi mkuu unapokaribia nchini, kwani wanasiasa huvunja na kubuni vyama na miungano ya kisiasa ambayo huwa haidumu hata kidogo.

Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (RPP) huwa yenye shughuli nyingi, wanasiasa na watu wenye ushawishi wakisajili vyama na miungano ya kisiasa kama matayarisho ya uchaguzi huo.

Ndiyo taswira iliyo katika afisi hiyo kwa sasa, kwani uchaguzi mkuu wa 2022 unaendelea kukaribia.

Kinaya huwa kwamba vyama hivyo hudumu mwa muda mfupi tu baada ya uchaguzi; vingine husahaulika au hata ‘kutupwa’ na wenyewe.

Mtindo huu ambao umekuwepo tangu 1992, umeifanya Kenya kuwa kama njia isiyoelekea kokote.

Hatuna falsafa yoyote maalum inayodhibiti siasa zetu hata kidogo!

Hatuna utambulisho kuhusu uhalisia wa siasa zetu. Ni siasa za pata potea, ambazo hazina mwongozo wowote maalum.

Kuyumbayumba huko ndiko kumetufanya kupitwa na nchi kama Tanzania, Afrika Kusini, Uingereza, Amerika kati ya mengine.

Licha ya matatizo madogo madogo yanayoiandama, Tanzania ina mfumo thabiti wa kisiasa kupitia vyama vikuu kama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na CHADEMA.

Afrika Kusini nayo ina mfumo wake maalum kupitia vyama kama African National Congress (ANC), Democratic Alliance (DA), Economic Freedom Fighters kati ya vingine.

Hata hivyo, Kenya ni kama nchi isiyojua inakoelekea kwani, hata vyama vichache vilivyopo huonekana kama “mali ya watu binafsi.”

Mfano maalum ni vyama vya ODM na Jubilee, ambapo ni dhahiri haviwezi kujisimamisha kisiasa bila uwepo wa Bw Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta mtawalia. Wao ndio ‘wamiliki’ wakuu wa vyama hivyo.

Chini ya mazingira kama hayo yanayodhibitiwa na watu fulani, ni vigumu kwa nchi kustawi au kukabili maovu yanayoiandama.

Hatuna lingine ila kujenga mfumo thabiti wa kisiasa, ikiwa tunalenga kurejesha hali ya uwajibikaji nchini.

akamau@ke.nationmedia.com

Habari zinazohusiana na hii