ONYANGO: Uhuru ameingia katika kipindi cha lala salama, atimize aliyoahidi

Na LEONARD ONYANGO

UMESALIA mwaka mmoja na miezi minane kabla ya Rais Uhuru Kenyatta kukamilisha muhula wake wa mwisho 2022.

Wakenya wanangojea kwa hamu na ghamu kuona miradi ambayo Rais Kenyatta aliahidi chini ya Ajenda Kuu Nne.

Mara baada ya kuapishwa kuongoza nchi kwa muhula wa pili mnamo Novemba 28, 2017, Rais Kenyatta aliahidi kuhakikisha kuwa kila Mkenya ananufaika na matibabu nafuu, anawezesha nchi kuwa na chakula cha kutosha, kuboresha viwanda na kuwasaidia maelfu ya Wakenya kupata makazi ya bei nafuu.

Lakini kufikia sasa ajenda hizo zingali zinachechemea na kuna dalili kwamba huenda rais akastaafu mwaka ujao bila kuzitimiza.

Miaka mitatu baada ya kutangaza ajenda hizo, sekta ya viwanda imedorora zaidi ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla yake kutwaa hatamu za uongozi wa nchi hii 2013.

Kwa mfano, ripoti ya msajili wa kampuni iliyotolewa 2019 ilionyesha kuwa jumla ya kampuni 388 zilifunganya virago na kuvunjiliwa mbali kati ya Machi na Agosti, mwaka huo, kutokana na kile wanauchumi wanasema hali ngumu ya uchumi.

Kutia msumari moto kwenye kidonda, janga la virusi vya corona limesababisha baadhi ya viwanda na kampuni kufungwa au kupunguza uzalishaji hivyo kuacha mamilioni ya Wakenya bila kazi.

Sekta ya afya ingali katika hali mbaya. Mnamo Desemba 13, 2018, Rais Kenyatta alizindua majaribio ya Mpango wa Matibabu Nafuu kwa Wote (UHC) katika Kaunti za Machakos, Kisumu, Nyeri na Isiolo.

Serikali ilitumia Sh3.9 bilioni kuhakikisha kuwa wakazi wa maeneo hayo wanatibiwa bure chini ya mpango wa UHC. Mpango huo ulifaa kuzinduliwa katika Kaunti zote Machi mwaka uliopita lakini serikali ikaahirisha kutokana na makali ya janga la virusi vya corona.

Kulingana wizara ya Afya, mpango huo utazinduliwa nchi nzima mwaka huu na kila familia itatakiwa kulipia Sh6,000 kila mwaka ili kunufaika na matibabu nafuu. Takribani Wakenya milioni 1 ambao ni maskini kupindukia watapata matibabu bila malipo.

Serikali haijafanya lolote kuboresha sekta ya kilimo ili kuhakikisha kuwa Kenya inakuwa na chakula cha kutosha. Nzige ambao wamekuwa wakivamia baadhi ya maeneo ya nchi hii na kuharibu mazao huenda wakasababisha Rais Kenyatta kuondoka mamlakani mwaka ujao na kuacha Wakenya wakihangaishwa kwa njaa.

Mwaka huu umesheheni shughuli tele za kisiasa – kama vile kampeni za uchaguzi mdogo wa ugavana wa Nairobi, kampeni za kura ya maamuzi ya Mpango wa Maridhiano (BBI) na siasa za urithi za 2022 – ambazo huenda zikasababisha rais kukosa wakati wa kushughulikia ahadi alizotoa kwa Wakenya.

Habari zinazohusiana na hii