• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Corona: Kanisa latishia kususia chanjo

Corona: Kanisa latishia kususia chanjo

Na WYCLIFFE NYABERI

VIONGOZI wa Kanisa Katoliki wametishia kuhimiza waumini wasusie chanjo ya kuepusha maambukizi ya virusi vya corona iwapo serikali haitatoa maelezo kamili kuhusu usalama wa chanjo hiyo kwa afya ya binadamu kabla ianze kutumika nchini.

Wito huo ulitolewa huku serikali ikijiandaa kupokea dozi za kwanza za chanjo ya virusi vya corona mwaka huu.

Viongozi hao wakiongozwa na Askofu Joseph Mairura wa Dayosisi ya Kisii, walisema licha ya Wakenya wengi kuonyesha nia ya kupokea chanjo hiyo, kuna baadhi ambao wana wasiwasi wa kuingiza mwilini kile wasichokifahamu.

Walikuwa wakizungumza katika misa iliyofanyika Nyabururu, Kisii jana Alhamisi.

Askofu Mairura alisema ipo haja ya hamasisho tosha kutolewa ili kuondoa hofu miongoni mwa raia.

Askofu huyo alisema iwapo serikali haitafanya vya kutosha kuwahakikishia kwamba chanjo hiyo haitakuwa na madhara yoyote baada ya kuitumia, basi watalazimika kuwashauri waumini wao kuisusia.

“Tunajua janga hili limesababisha madhara mengi katika uchumi wetu na wengi wanataka kurejea katika hali yao ya kawaida. Lakini hatuwezi kuharakisha kukubali mambo bila kuelezwa kikamilifu. Lazima tujue kisayansi chanjo hii ni nzuri la sivyo tutaisusia, ” akasema Askofu Mairura.

Aidha, kiongozi huyo aliwasihi wakongwe kujilinda vilivyo ili wasiambukizwe maradhi hayo yanayowaua kwa kasi. Mnamo Disemba, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alidokeza kwamba, serikali imeagiza dozi millioni 24 za chanjo ya Oxford-AstraZeneca ambayo itawasili nchini kufikia Aprili 2021.

Waziri Kagwe aliongeza kuwa chanjo ya Oxford ilikuwa ya bei nafuu ikilinganishwa na chanjo zingine ambazo zimevumbuliwa.

“Wizara ya afya pamoja na taasisi ya KEMRI zinazidi kufanya majaribio. Chanjo ya Oxford-AstraZeneca inaweza kuhifadhiwa virahisi katika barafu za kawaida ikilinganishwa na zingine,” Bw Kagwe akaeleza kwenye mahojiano ya awali.

Uchanjaji utakapoanza, watu wanaokisiwa kuwa kwenye hatari ya kuambukizwa virusi hivyo, hasa wale wanaotangamana na halaiki ya watu ndio wa kwanza watakaoipokea.

You can share this post!

Watoto watano wafariki baada ya kutumbukia katika shimo la...

Hatuna mpango wa kuuza Origi – Liverpool