• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 10:10 AM
Covid-19 yaunyima mwaka 2021 makaribisho ya haiba

Covid-19 yaunyima mwaka 2021 makaribisho ya haiba

Na SAMMY WAWERU

KWA kawaida miaka ya awali makaribisho ya mwaka mpya yamekuwa yakisheheni mbwembwe, vifijo na nderemo kwa wanaokusanyika maeneo mbalimbali kuulaki.

Wananchi wamekuwa wakikusanyika katika maeneo ya kuabudu, vilabu na maeneo ya burudani, shangwe na fataki zikitawala anga kuukaribisha.

Makaribisho ya 2021 hata hivyo yamekuwa tofauti kabisa na taswira hiyo.

Sheria na mikakati iliyowekwa na serikali kusaidia kuzuia maenezi ya virusi vya corona (Covid-19), zililazimu wananchi kuulaki wakiwa nyumbani.

Amri ya kafyu ya kitaifa inayoanza kutekelezwa saa nne usiku na marufuku ya mikusanyiko ya umma isingeruhusu Wakenya kuendeleza mila na utamaduni wa makaribisho ya mwaka mpya.

Ikizingatiwa kuwa corona ni janga la kimataifa, mengi ya mataifa ulimwenguni pia yalilazimika kubadili tamaduni zake kuikaribisha 2021.

Covid-19 yaunyima mwaka 2021 makaribisho ya haiba. Picha/ Sammy Waweru

Alhamisi, Desemba 31, 2020, saa nne kamili zilipotimia, maafisa wa usalama nchini walikuwa ange kutekeleza amri ya kafyu.

Kwenye hotuba yake kabla ya maadhimisho ya Krismasi 2020, Inspekta Mkuu, IG, Hillary Mutyambai aliweka wazi kuwa sheria za corona sharti ziheshimiwe.

“Kafyu inaanza saa nne kamili, hakikisha umeingia kwenye nyumba kabla ya saa hizo kutimia,” akaonya IG Mutyambai.

Alhamisi jioni, jiji la Nairobi na viunga vyake, wakazi walijikakamua kuhakikisha wanarejea makwao kabla ya muda wa kafyu kutimia.

Dakika kadha baada ya saa nne, barabara nyingi zilikuwa mahame, wanaoonekana wakipita wakiwa mmoja mmoja hasa waliobebwa na wanabodaboda.

Licha ya amri ya kafyu, ilipotimia saa sita usiku, wananchi walijitokeza kwenye roshani za majengo wanayoishi kuikaribisha 2021 kwa shangwe, vifijo na nderemo na kufyatua fataki.

Wahudumu kadha wa bodaboda eneo la Thika Road walijitokeza katika barabara za mashinani, ila kwa uangalifu wasikumbane na mkono wa sheria.

Wachangiaji wa mitandao ya kijamii nao walielekeza heri njema za mwaka mpya mitandaoni.

 

  • Tags

You can share this post!

Obiri atamalaki mbio za Cursa dels Nassos nchini Uhispania...

Messi atamani kucheza soka Amerika kabla ya kurejea...