Pochettino kushawishi PSG kurefusha mikataba ya Neymar na Mbappe kabla ya kusajili Lloris, Alli na Eriksen

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI Mauricio Pochettino amesema kubwa zaidi katika malengo atakapotwaa mikoba ya Paris Saint-Germain (PSG) ni kushawishi usimamizi wa miamba hao wa soka ya Ufaransa (Ligue 1) kurefusha mikataba ya wanasoka Neymar na Kylian Mbappe.

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe, Pochettino anatarajiwa kukutana na vinara wa PSG wikendi hii kabla ya kutia wino kandarasi atakayopokezwa kwa kuwa tayari kocha huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur ameafikiana nao.

Pochettino ambaye alichezea PSG kati ya 2001 na 2003, ndiye atakayekuwa sasa mrithi wa mkufunzi Thomas Tuchel aliyetimuliwa ugani Parc des Princes mnamo Disemba 24, 2020.

Zaidi ya kutaka PSG warefushe mikataba ya Neymar na Mbappe, Pochettino atapania pia kushawishi waajiri wake wapya kujinasia huduma za wanasoka Dele Alli, Hugo Lloris na Christian Eriksen aliowahi kuwanoa kambini mwa Spurs.

Huku dalili zote zikiashiria kwamba Alli amekosekana katika mipango ya baadaye ya kocha Jose Mourinho kambini mwa Spurs, Inter Milan ya Italia tayari wameanika mipango ya kumtia Eriksen mnadani baada ya nyota yake kutong’aa uwanjani San Siro.

Neymar aliyetua PSG kwa kima cha Sh26 bilioni mnamo 2017 anahusishwa na uwezekano wa kurejea Barcelona huku Mbappe akiwaniwa pakubwa na Real Madrid walioanza kuyahemea maarifa yake hata kabla abanduke kambini mwa AS Monaco.