• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Kibarua kigumu kwa wanavoliboli wa Kenya kimataifa baada ya CAVB kutoa ratiba ya msimu wa 2021

Kibarua kigumu kwa wanavoliboli wa Kenya kimataifa baada ya CAVB kutoa ratiba ya msimu wa 2021

Na CHRIS ADUNGO

TIMU za Kenya zitakuwa na kampeni nzito katika mchezo wa voliboli msimu ujao wa 2020-21 kwa mujibu wa kalenda mpya iliyotolewa na Shirikisho la Voliboli barani Afrika (CAVB) mnamo Januari 1, 2021.

Katika ratiba hiyo, mashindano ya kwanza yatakuwa ya kuwania Kombe la Afrika kwa wasichana wasiozidi umri wa miaka 20 na vigoli wasiozidi umri wa miaka 18. Mapambano hayo yataandaliwa nchini Uganda na Nigeria mtawalia kati ya Januari 26 na Februari 7, 2021.

Kipute cha wavulana wasiozidi umri wa miaka 19 kitafanyika nchini Tunisia kati ya Februari 1-6 kabla ya kile cha mabarobaro wasiozidi umri wa miaka 21 kuandaliwa Misri mnamo Februari 18-26.

Mapambano ya kuwania taji la Afrika miongoni mwa klabu za wanawake yatafanyika kati ya Machin a Aprili katika nchi itakayofichuliwa na CAVB baadaye mwezi ujao. Vikosi vya Kenya vimekuwa vikijivunia matokeo ya kuridhisha sana kwenye kivumbi hicho katika miaka ya hivi karibuni.

Kinyang’anyiro hicho kitaendeshwa sambamba na kile kitakachoshirikisha vikosi vya wanaume. Mwenyeji wa kipute hicho atafichuliwa pia na CAVB mwakani.

Mwishoni mwa wiki jana, Shirikisho la Voliboli la Kenya (KVF) lilithibitisha kwamba kampeni za Ligi Kuu katika msimu wa 2020-21 sasa zitaanza mnamo Januari 23 baada ya kivumbi hicho kusimamishwa kuanzia Juni 2020 kwa sababu ya janga la Covid-19.

Kufikia sasa, timu nane za voliboli ya wanawake na 13 kwa upande wa wanaume zimesajiliwa kunogesha kinyang’anyiro hicho kitakachowiana na mfumo wa Shirikisho la Voliboli ya Kimataifa (FIVB).

Ingawa hivyo, kwa kuwa idadi ya vikosi ambavyo vimejisajilisha kwa ligi hiyo ni ndogo, kampeni zenyewe za muhula ujao zitakamilisha baada ya muda mfupi.

“Vikosi vya wanawake ambavyo vimethibitisha ushiriki wao kufikia sasa ni pamoja na Kenya Defence Forces, Kenya Army, Kenya Prisons, Directorate of Criminal Investigations (DCI), Prison Nairobi, Nairobi Water, KCB na Kenya Pipeline,” akasema Afisa wa Mawasiliano wa KVF, Isaac Tirop.

Katika kitengo cha wanaume, mabingwa watetezi GSU watatoana jasho na KDF, Forest Rangers, Kenya Prisons, Prisons Nairobi, Western Rangers, Equity, Rift Valley Prison, Vihiga, Kenya Army, Administration Police, Kenya Ports Authority na Prisons Mombasa.

Kwa mujibu wa mfumo wa FIVB, timu 16 zinatarajiwa kushiriki raundi ya kwanza ya mchujo ambapo vikosi vitatiwa kwenye makundi manne ya timu nne.

Kila timu itacheza dhidi ya nyingine kundini mara mbili ambapo vikosi vitatu vya kwanza vitatiwa kwenye makundi mawili kwa minajili ya raundi ya pili ya mchujo. Mechi za hatua hii zitakuwa pia za mikondo miwili, kila kikosi kikichezea nyumbani na ugenini.

Kwa mujibu wa Tirop, KVF inapania kutafuta viwanja vingine vya ziada zitakavyotumiwa na vikosi vya Ligi Kuu ya Voliboli baada ya Kamati Kuu ya Kitaifa ya Olimpiki (NOC-K) kutwaa uga wa MISC Kasarani kwa minajili ya mazoezi ya Team Kenya inayojiandaa kwa Olimpiki za Tokyo, Japan.

Timu ya taifa ya wanawake almaarufu Malkia Strikers itanogesha michezo hiyo ya Olimpiki iliyoahirishwa hadi Julai 2021 kwa sababu ya corona.

Baada ya kukamilisha kampeni za Olimpiki, Malkia Strikers watatarajiwa kushiriki kipute cha kuwania ubingwa wa bara Afrika kabla ya kuanza kuwinda tiketi ya fainali za Kombe la Dunia za 2022 kuanzia Agosti kabla ya kuanza kampeni za kufuzu kwa Olimpiki za 2024 jijini Paris, Ufaransa.

Mkurugenzi Mkuu wa KVF David Lung’aho na Kaimu Mwenyekiti ya Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (NOC-K) Francis Mutuku, wamethibitisha kwamba Malkia Strikers watarudi uwanjani kwa mazoezi kuanzia mwezi ujao.

Lung’aho amesema janga la corona limetatiza juhudi za Malkia Strikers kujinasia huduma za wanavoliboli wapya msimu huu kwa kuwa vikosi vya Ligi Kuu hutegemea wachezaji kutoka shule za msingi na upili ambazo zimefungwa kwa muda mrefu kutokana na Covid-19.

Kwa kipindi cha miaka mingi, Malkia Strikers imekuwa ikitegemea idadi kubwa ya wachezaji kutoka Shule za Kwanthanze Girls na Lugulu Girls huku Lelmokwo, Mogonga High na Sengera zikichangia idadi kubwa ya wachezaji kwa vikosi vya Ligi Kuu na timu ya taifa ya voliboli kwa upande wa wanaume almaarufu Wafalme.

You can share this post!

Baraza la viongozi wa kidini kuhusu Covid-19 laongezewa...

Dereva wa magari ya langalanga Lewis Hamilton sasa atakuwa...