• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Wazazi Thika wafurika madukani kuwanunulia watoto wao sare, vifaa vya shuleni

Wazazi Thika wafurika madukani kuwanunulia watoto wao sare, vifaa vya shuleni

Na LAWRENCE ONGARO

WAZAZI wengi walifurika katika duka za kuuza sare za shule na viatu kwa matayarisho ya kurejea kwa wanafunzi masomoni.

Baadhi ya wazazi waliohojiwa wanasema ya kwamba hali ngumu ya maisha inawatatiza na wanajikaza tu kisabuni.

Wengine walisema ya kwamba waliachishwa kazi wakati huu wa janga la corona.

Bi Ruth Okapi aliyehojiwa na Taifa Leo alisema anajitayarisha kupeleka mwanaye asome shule ya chekechea.

“Sisi kama wazazi tunapitia hali ngumu lakini tutajikaza tu ili watoto wetu wasome. Wengi wetu hatuna ajira kwa sasa,” akasema Bi Okapi.

Naye Bi Monica Wanjohi alisema watajaribu wawezavyo kuona ya kwamba watoto wao wanabeba barakoa na sanitaiza ili waweze kukabiliana na corona.

“Hata hivyo, ni vyema serikali ijitokeze ili iweze kuweka mikakati kamili hasa wakati huu shule zinapofunguliwa,” alisema Bi Wanjohi.

Mfanyakazi katika duka la Chania School Depot Bi Julia Nduta anasema biashara ni ya chini sana wakati huu ikilinganishwa na hapo awali.

“Wazazi wengi hawana hela ya kutosha kutokana na yale wamepitia kwa zaidi ya miezi tisa. Tunaelewa maisha ni magumu,” alisema Bi Nduta.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alipohojiwa alisema wakuu wa shule wana kibarua hasa wakati huu wanafunzi wanarejea masomoni kwa fujo.

“Jambo muhimu kwa sasa ni kuona ya kwamba kuna maji ya kutosha na madarasa zaidi kuongezwa,” alisema Bw Wainaina.

Alisema atafanya juhudi kuona ya kwamba eneo lake la uwakilishi linaongeza madarasa kadha shuleni ili kutosheleza mahitaji ya wanafunzi.

Alisema atafanya mipango kuona ya kwamba shule kadha za msingi zinapokea barakoa na sabuni kwa wingi.

“Hata ingawa Covid-19 bado iko miongoni mwetu itabidi wanafunzi warejee masomoni huku sheria za Wizara ya Afya zikifuatwa jinsi ipasavyo,” alisema mbunge huyo.

Alieleza kuwa nchi za ng’ambo kama Uswidi na Amerika zimerejesha wanafunzi shuleni licha ya Covid-19 kuwepo.

Alisema katika shule za msingi kutakuwepo na watu maalum watakaokuwa mstari wa mbele kufunza maswala ya Covid-19 ili kila mmoja, wanafunzi na walimu wawe na ufahamu wa jinsi ya kukabiliana na janga hilo.

Alisema huu ni wakati wa kila mmoja kuwa mstari wa mbele kujichunga kuepuka Covid-19.

Hivi majuzi serikali ilipendekeza kuwa itabidi wanafunzi wengine kusomeshewa nje ya madarasa yao ikiwemo chini ya miti kwenye kivuli.

  • Tags

You can share this post!

Covid-19 yavuruga maandalizi ya timu ya taifa ya Zimbabwe...

Mwanamasumbwi Rayton Okwiri atemwa kwenye kikosi cha Hit...