• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 10:55 AM
Mikasa ya kufa maji yatamatisha 2020

Mikasa ya kufa maji yatamatisha 2020

Na WAANDISHI WETU

MIKASA ya vifo vilivyotokana na watu kufa maji viliripotiwa katika maeneo tofauti ya nchi mwisho wa mwaka jana na mkesha wa 2021.

Maafa ya kwanza yalitokea katika eneo la Mwihoko eneobunge la Ruiru, Kiambu ambapo watoto watano waliaga dunia baada ya kutumbukia kwenye tanki ya futi 20 iliyojaa maji.

OCPD wa Ruiru Phineas Lingera alieleza Taifa Leo kwamba, watoto hao walikuwa na umri wa kati ya miaka mitatu hadi saba na walikuwa wakicheza karibu na tanki hiyo ambayo ilikuwa imefunikwa na nyasi.

Inakisiwa watoto hao walifariki baada ya kushindwa kupumua ndani ya tangi.

“Walikuwa wakicheza karibu na eneo ambako ujenzi ulikuwa ukiendelea ambapo mstawishaji moja anajengea nyumba. Pia kuna choo ambacho kinajengwa eneo hilo na huenda watoto hao walikanyaga nyasi iliyofunika tangi hiyo kisha kutumbukia ndani,” akasema Bw Lingera.

Miili ya watano hao ilipelekwa katika mochari ya hospitali ya Chuo Kikuu cha Kenyatta. Kwenye kisa kingine, mtaani Huruma, Njoro, Kaunti ya Nakuru mwanamume mwenye umri wa miaka 37 alimdunga mpenziwe kwa kisu hadi akamuua siku ya mwisho ya mwaka 2020.

Mwanamume huyo Joseph Kipkirui alimdunga kwa kisu mpenziwe Purity Mumbi, 22 mara tano katika nyumba yao mjini Njoro. Bw Kipkirui kisha alijisalimisha katika kituo cha polisi cha Njoro na kukiri kutekeleza mauaji hayo.

Kulingana na Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Njoro, Jonathan Kisaka, Bw Kipkirui aliandamana na polisi hadi nyumba yake ambako mwili wa Bi Mumbi ulipatikana ukitoka damu. Katika Kaunti ya Kilifi, watu wawili walifariki baada kuzama katika kidimbwi cha maji cha kunywesha mifugo cha Mukuluni kata ya Kayafungo eneobunge la Kaloleni.

Kamanda wa polisi wa eneobunge hilo Ezekiel Chepkwony alisema wawili hao walizama siku mbili tofauti, Jumatano na Alhamisi. Mkasa mwingine ulitokea Kaunti ya Kisumu baada ya mwili wa mwanaume aliyekuwa akizoa mchanga kwenye fuo ya Ngege, Korando kupatika ukiielea majini.

Ripoti za SIMON CIURI , ERIC MATARA, MAUREEN ONGALA NA RUSHDIE OUDIA

You can share this post!

Walevi wakesha waumini wakilala

TAHARIRI: Kuwe na ari ya kufufua spoti