TAHARIRI: Kuwe na ari ya kufufua spoti

KITENGO CHA UHARIRI

MWAKA huu mpya wa 2021 unatarajiwa kuwa wa kipekee nchini katika nyanja ya michezo huku wanaspoti wetu wakishiriki mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Jambo la muhimu zaidi tunapojitayarisha kushiriki mashindano hayo ni kwa serikali kuwapa usaidizi wa kutosha wanaspoti wetu wanapojitahidi kuiletea nchi yetu sifa kedekede.

Hii ni kwa sababu mashindano mengi yaliyoahirishwa mwaka 2020 sababu ya janga la virusi vya corona, sasa yatafanyika mwaka huu 2021.

Shindano kubwa zaidi 2021 litakuwa michezo ya Olimpiki jijini Tokyo, Japan. Michezo hiyo ilikuwa imeratibiwa kufanyika kuanzia Julai 24 hadi Agosti 9, 2020, lakini ikatangazwa kuahirishwa mapema mwezi Machi kutokana na mkurupuko wa corona.

Sasa mashindano hayo, ambayo Kenya imekuwa ikijizolea medali fufu, yataandaliwa Julai 25 hadi Agosti 8, 2021.

Kenya itawasilishwa katika fani ya mbio, uogelaji, raga na voliboli. Mazoezi kwa Team Kenya yataanza rasmi ugani Kasarani mnamo Julai 10.

Kenya pia itakuwa mwenyeji wa mashindano ya mbio za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 barani Afrika, kati ya Agosti 17-22 mwaka huu uwanjani Nyayo. Kenya inapigiwa upatu kung’aa katika riadha hizo ikizingatiwa zitaandaliwa nyumbani.

Katika fani ya soka, yenye mashabiki lukuki nchini, timu ya taifa Harambee Stars itachuana na Misri mnamo Machi 22 jijini Nairobi. Kisha vijana wa nyumbani watavaana na Togo mnamo Machi 30 kwenye mechi ya kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Bara Afrika.

Stars itakuwa na kibarua kigumu hasa baada ya kujikwaa dhidi ya Kisiwa cha Comoros mwaka 2020, japo kutakuwa na tumaini iwapo wanavisiwa hao watapoteza dhidi ya Togo na Misri.

Kwenye mechi za klabu bingwa Afrika (CAF), mabingwa wa ligi kuu nchini, Gor Mahia, watahitaji muujiza katika mechi ya marudiano dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria wiki ijayo siku ya Jumatano.

K’Ogalo wanafaa kufunga mabao saba bila jibu katika mechi hiyo ili kusonga mbele, baada ya kukalifishwa 6-0 kwenye mechi ya mkondo wa kwanza Desemba 2020 jijini Algiers.

Shindano lingine la hadhi ambalo linasubiriwa kwa hamu ni kurejea kwa mbio za magari za Safari Rally, ambazo zilifanyika mara ya mwisho nchini miaka 19 iliyopita. Safari Rally zitafanyika tena Juni 24-27 na zinatarajiwa kushirikisha madereva wa humu nchini na nje.

Habari zinazohusiana na hii