WASONGA: Serikali igharimie kuunda maski za kuwatosha wanafunzi

Na CHARLES WASONGA

ELIMU ni chombo muhimu cha kuziba pengo kati ya maskini na tajiri kwa taifa linaloendelea kama Kenya.

Hivyo, ni wajibu wa serikali kuhakikisha wanafunzi wote, haswa kutoka jamii maskini, wanapata nafasi ya kusoma sawa na wenzao kutoka jamii zenye uwezo kifedha.

Shule zinapofunguliwa tena Jumatatu, serikali inafaa kuhakikisha kuwa wanafunzi kutoka jamii maskini wanapata vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi ya Covid-19, mathalan, barakoa.

Japo Waziri wa Elimu Prof George Magoha amesema Wizara itawapa wanafunzi wasiojiweza maski bila malipo, duru zinadai kuna uhaba wa barakoa milioni moja zilizonuiwa kupewa wanafunzi hao.

Awali, Prof Magoha alikuwa ametangaza kuwa Wizara ya Elimu ingesambaza barakoa milioni tatu kwa wanafunzi ambao hawawezi kumudu gharama ya vifaa hivyo.

Hii ni baada ya kung’amua kuwa imefeli kupanua miundomsingi shuleni, kupitia ujenzi wa madarasa mapya, ili kupunguza misongamano haswa katika shule za umma.

Nyingi ya shule zisizo na madarasa ya kutosha zinapatikana katika maeneo kame na yenye changamoto mbalimbali za kimaumbile.

Kwa hivyo, serikali inapasa kuipa kampuni ya kutengeneza nguo ya Rivatex mjini Eldoret, kazi ya kuunda idadi inayohitajika ya maski kwa ajili ya kusambazia wanafunzi kutoka jamii maskini.

Vile vile, serikali iwape mafundi wa jua kali kazi ya kutengeneza vifaa hivyo kwa gharama nafuu, ilivyofanya chini ya mpango wa utengenezaji madawati iliyogharimu Sh1.9 bilioni.

Wizara ya Elimu kamwe haina sababu ya kudai upungufu wowote wa barakoa milioni moja za kuwapa wanafunzi, ilhali serikali imekuwa ikiipa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pesa za kufadhili mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) na pia chaguzi ndogo.

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), watoto walio na miaka 12 na zaidi wanahitaji kuvaa maski ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, katika maeneo ambako ni vigumu watu kukaa mbali.

WHO inaongeza kuwa, watoto walio chini ya miaka 12 wanafaa kuvalia barakoa kwa kuwa katika hatari zaidi ya kuambukizwa virusi vya corona.

Hivyo, ikizingatiwa kuwa serikali iliwataka wazazi na wadau wengine kuwaandaa wanafunzi kwa ufunguzi wa shule, nayo pia isiwe ya kuchelea katika kutimiza wajibu wake wa kuwasaidia wanafunzi wanaotoka jamii maskini kupewa kila usaidizi wanaohitaji kupata masomo.

Aidha, amri ambayo serikali ilitoa kwa machifu na maafisa wengine wa utawala, kuhakikisha kuwa watoto wote wanaripoti shule Jumatatu, inafaa kuandamana na jitihada kabambe kuhakikisha wanafunzi wote na kote nchini wanarejea darasani.

Habari zinazohusiana na hii