MUTUA: Weka mipango ya maisha sio tu maazimio ya mwaka

Na DOUGLAS MUTUA

WAKATI huu si watu wengi wamekuwa jasiri kutangaza maazimio yao ya mwaka mpya wa 2021.

Kipindi kama hiki mwaka jana, mitandao ya kijamii ilijaa kila aina ya maazimio, watu wakieleza wazi waliyotaka wayaafikie kabla ya mwaka 2020 kuisha.

Tunakubaliana kwamba 2020 ulikuwa mgumu katika mambo mengi, lakini ugumu huo ulizidishwa na janga la virusi vya corona.

Hata walioshindwa kuafikia maazimio yao kwa sababu ya uzembe au kukosa mipango endelevu, walipata kisingizio: corona.

Ni kwa mintaarafu hiyo ambapo kauli kama ‘tutaona baada ya corona’ iliibukia kuwa maarufu sana; kawaida ya Wakenya wakiahidi kutimiza ahadi walizotoa janga likiondoka.

Kwa bahati mbaya kwa watu waliotoa kisingizio cha corona, janga lenyewe limekataa kuondoka huku shughuli za kiuchumi zikisitishwa kabla kurejelewa tena baada ya miezi kadha.

Bila shaka waliopumbazwa kwa ahadi za uongo walichoka na kujanjaruka, waongo hao wakaingia mashakani; ama ahadi zikatimizwa na madeni yakalipwa, au watu wakala huu na hasara juu.

Mwaka huu, hata wanamuziki wa janibu za Ukambani ambao hawachelewi kufyatua vibao vipya vinavyoendana na wakati, wamekuwa waangalifu sana wasitabiri mambo ya kunoa.

Kwa maoni yangu, maazimio ya mwaka mpya yanapaswa kuwa nyongeza tu ya mpango mzima wa maisha ya mtu, si mpango mzima wenyewe.

Ukiweka matumaini yako yote katika maazimio ya mwaka mpya, unaweza kupata msongo wa mawazo iwapo hutayaafikia.

Kwa mfano, wanafunzi wa darasa la nane na kidato cha nne waliopanga kukamilisha masomo yao mwaka jana yawezekana wakahuzunika sana na kusahau kwamba bado watafanya mitihani ya kitaifa.

Wazazi wao pia wanaweza kuzugika akili kutokana kwamba jitihada za kuelimisha wana wao vyuoni na sekondari ziligonga mwamba.

Kumbuka baadhi ya wazazi waliishia kula karo ya shule taasisi hizo zilipofungwa ghafla kutokana na corona. Kisha ghafla serikali ikawaagiza watoto wao warejee shuleni kuendelea na masomo ya darasa la nane na kidato cha nne.

Inaeleweka. Pesa, japo ni akiba isiyooza, zina mwasho wa aina yake zikiwa mfukoni!

Kwa maoni yangu, lengo kuu la mwanafunzi linapaswa kuwa kuanza na kumaliza masomo ya ngazi fulani hata ikiwa atalazimika kurudia darasa moja mara nne!

Azimio lake la muda nalo lafaa kuwa atapiga hatua fulani masomoni, akishindikana anarudi alikoanzia na kujaribu mbinu nyingine kama mwindaji aliyelenga bila kufuma.

Naambiwa kuvunjika kwa mwiko si mwisho wa kupika sima. Hata ikiwa mipango yako ya maisha itacheleweshwa na corona ama ukosefu wa fedha, nia yako inapaswa kuwa: utaitekeleza liwe lilwalo, bila kujali utatumia muda gani.

Corona imetukumbusha kuwa usafi ni kiungo muhimu sana ili kuepuka viini vya maradhi.

Hii ni fursa bora kwa maafisa wa afya ya jamii kutekeleza malengo ya muda mrefu ya serikali kuhusu afya njema, kama vile kuhakikisha kila familia ina choo na maji safi ya kunywa.

mutua_muema@yahoo.com

 

Habari zinazohusiana na hii