• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Arsenal watangaza rasmi ufufuo wao ligini kwa kupokeza West Brom kichapo kinono cha 4-0 ugenini

Arsenal watangaza rasmi ufufuo wao ligini kwa kupokeza West Brom kichapo kinono cha 4-0 ugenini

Na MASHIRIKA

ARSENAL waliendeleza ufufuo wao kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kuwapokeza West Bromwich Albion kichapo cha 4-0 mnamo Jumamosi usiku uwanjani The Hawthorns.

Beki Kieran Tierney aliwaweka Arsenal kifua mbele katika dakika ya 23 kabla ya Bukayo Saka kushirikiana vilivyo na Alexandre Lacazette na Emile Smith-Rowe na kucheka na nyavu za wenyeji wao kunako dakika ya 28 na kufanya mambo kuwa 2-0.

Lacazette alifungia Arsenal bao la tatu katika dakika ya 60 baada ya kupokezwa krosi na Smith-Rowe kabla ya kujaza kimiani goli la nne la waajiri wake dakika nne baadaye kutokana na pasi ya Tierney.

Ilikuwa mara ya tatu mfululizo kwa Arsebal kushinda mechi ya EPL msimu huu baada ya juhudi zao kutozaa matunda katika msururu wa michuano saba ya awali.

West Brom waliokuwa wakisakata mchuano wao wan ne chini ya kocha mpya Sam Allardyce walisalia katika nafasi ya 19 kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama nane, sita pekee mbele ya Sheffield United wanaovuta mkia.

Arsenal waliingia uwanjani wakitawaliwa na motisha ya kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakizamisha vyombo vya Chelsea na Brighton kwa vichapo vya 3-1 na 1-0 katika mechi mbili za awali.

Hector Bellerin alimweka kipa Sam Johnstone katika ulazima wa kufanya kazi ya ziada mwanzoni mwa kipindi cha kwanza baada ya Pierre-Emerick Aubameyang kumpokeza beki huyo raia wa Uhispania pasi nzuri iliyomwacha hoi beki Dara O’Shea.

Baada ya kuona uhakika wa kikosi chake kutia kapuni alama tatu muhimu kutokana na mchuano huo, kocha Mikel Arteta aliwapumzisha chipukizi wake tegemeo Saka na Smith-Rowe na badala yake kuwaleta uwanjani Joe Willock, Willian Borges na Ainsley Maitland-Niles aliyejaza nafasi ya Hector Bellerin.

Mchuano wa kwanza wa Allardyce kambini mwa West Brom ulikamilika kwa kichapo cha 3-0 kutoka kwa Aston Villa baada ya nahodha Jake Livermore kuonyeshwa kadi nyekundu.

Hata hivyo, walijitosa ugani dhidi ya Arsenal wakitarajiwa kujinyanyua baada ya kuwalazimishia Liverpool ambao ni mabingwa watetezi wa EPL sare ya 1-1 katika mchuano wa awali kabla ya limbukeni Leeds United kuwaponda 5-0 ugani The Hawthorns mnamo Disemba 29, 2020.

West Brom ndicho kikosi cha kwanza baada ya Wigan mnamo Agosti 2010, kuwahi kupoteza mechi mbili za EPL katika uwanja wa nyumbani kwa angalau mabao manne katika kila moja.

West Brom kwa sasa wanatarajiwa kuchuana na Blackpool ugenini katika mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA mnamo Januari 9 kabla ya kurejelea kampeni za EPL kwa kuvaana na Wolves mnamo Januari 16.

Kwa upande wao, wataanza utetezi wa Kombe la FA dhidi ya Newcastle ugani Emirates mnamo Januari 9 kabla ya kuwaalika Crystal Palace kwa gozi la EPL mnamo Alhamisi ya Januari 14, 2021.

You can share this post!

Real Madrid watandika Celta Vigo ugani Bernabeu na kurejea...

Brighton watoka nyuma kwa mabao 3-1 na kulazimisha sare ya...