• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
PSG wamwajiri kocha Pochettino kwa mkataba wa miezi 18

PSG wamwajiri kocha Pochettino kwa mkataba wa miezi 18

Na MASHIRIKA

KOCHA Mauricio Pochettino, 48, amepokezwa rasmi mikoba ya kikosi cha Paris Saint-Germain (PSG) cha Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) kwa mkataba wa miezi 18.

Mkufunzi huyo raia wa Argentina hakuwa na kazi tangu alipotimuliwa na Tottenham Hotspur ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Novemba 2019 na atakuwa huru kurefusha kandarasi yake kambini mwa PSG kutegemea matokeo atakayosajili.

Licha ya kuhusishwa na mikoba ya vikosi vingi vya bara Ulaya hapo awali vikiwemo Real Madrid na Barcelona, Pochettino alihiari kuyoyomea Ufaransa kuwa mrithi wa Mjerumani Thomas Tuchel aliyetimuliwa na PSG mnamo Disemba 24, 2020 licha ya kuongoza waajiri wake kupepeta Strasbourg 4-0 ligini.

Baada ya kutimuliwa kwa Tuchel, PSG walifanya hima na kuanza kumshawishi Pochettino kudhibiti mikoba yao. Kocha huyo aliwahi kuchezea PSG kati ya 2001 na 2003 akiwa nahodha wa kikosi.

Pochettino aliwasili rasmi katika makao makuu ya PSG jijini Paris, Ufaransa mnamo Jumamosi kurasimisha kuajiriwa kwake na wanafainali hao wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) waliopigwa 1-0 na Bayern Munich mwishoni ma msimu wa 2019-20 jijini Lisbon, Ureno.

“Karibu sana Pochettino. Tuna fahari ya kutangaza kwamba Pochettino kwa sasa ndiye kocha wetu rasmi. Ametia saini mkataba wa miezi 18 ambao utatamatika mnamo Juni 30, 2022 japo atakuwa huru kurefusha kandarasi hiyo,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na PSG.

“Ni tija tele kupokezwa mikoba ya PSG ambao niliwahi kuwachezea katika miaka yangu ya usogora. Najua matarajio ya kila mtu ni makubwa uwanjani Parc des Princes. Naamini tutafaulu pamoja kupeleka kikosi mahali ambapo kinastahili kuwa katika soka ya bara Ulaya,” akasema Pochettino.

Kwa upande wake, Nasser Al-Khelaifi ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa PSG alisema: “Tuna furaha kubwa kumkaribisha Pochettino, nahodha wetu wa zamani ambaye kwa sasa ni kocha. Anarejea katika kikosi anachokifahamu vyema kwa sababu anaelewa falsafa ya PSG.”

Pochettino kwa sasa atasaidiwa na wakufunzi Jesus Perez na Miguel D’Agostino waliokuwa wasaidizi wake kambini mwa Spurs.

Mchuano wa kwanza ambao Pochettino anatarajiwa kusimamia kambini mwa PSG ni gozi la Ligue 1 litakalowakutanisha na Saint-Etienne mnamo Januari 6, 2021.

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe nchini Ufaransa, Pochettino anatarajiwa kuandaa kikao cha kwanza na wanasoka wa PSG mnamo Disemba 3, 2021 uwanjani Parc des Princes.

Kati ya mikakati ambayo Pochettino anatarajiwa kushawishi usimamizi wa PSG kutekeleza ni kurefusha mikataba ya nyota Neymar Jr na Kylian Mbappe kabla ya kusajiliwa kwa wanasoka Hugo Lloris, Dele Alli na Christian Eriksen. Neymar na Mbappe wanahemewa pakubwa na Barcelona na Real Madrid mtawalia.

You can share this post!

Palace wafunga mawili na kuendeleza masaibu ya Sheffield...

Limbukeni Kiprop na Chirchir watamalaki Mbio za Nyika za AK...