• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Wachangiaji mitandao waliofunga pingu za maisha wachangamka kueleza safari yao kwenye ndoa kupitia kundi jipya la Thriving Couples KE

Wachangiaji mitandao waliofunga pingu za maisha wachangamka kueleza safari yao kwenye ndoa kupitia kundi jipya la Thriving Couples KE

Na SAMMY WAWERU

WACHANGIAJI maoni katika mitandao ya kijamii wanaendelea kuridhia kundi jipya la Facebook lililobuniwa kwa minajili ya wanandoa kueleza mafanikio kwenye ndoa yao.

Kundi hilo maarufu kama Thriving Couples KE, baadhi ya wanandoa – wachangiaji wa Facebook wamekuwa wakichapisha maelezo kuhusu walivyopatana na wachumba wao, safari yao kwenye ndoa, yakiandamana na picha za matukio.

Kufikia sasa, kundi hilo lililofunguliwa mwaka uliopita, Oktoba 11, 2020, lina zaidi ya wachangiaji 602, 000 wanaolifuatilia.

Baadhi ya wanandoa waliofunga pingu za maisha ipatayo miaka 30, 20, 15, 10, 5, iliyopita na wengine miezi kadha wamejitosa Thriving Couples KE wakisimulia milima, mabonde, miteremko na mafanikio kwenye uhusiano wao.

Gibson Gathu Mbugua, aliyekuwa mwigizaji maarufu katika kipindi cha Vioja Mahakamani, kama kiongozi wa mashtaka ya umma kortini, kinachopeperushwa na runinga ya KBC, ni kati ya wanandoa waliojitokeza.

“Miaka 30 iliyojaaliwa baraka kwenye ndoa,” Gathu akachapisha katika kundi hilo mnamo Desemba 17, 2020 maelezo hayo yakiandamana na picha anayoonekana na mkewe.

Aidha, chapisho hilo lilivutia zaidi ya michango 4, 000 ya maoni.

“Hongera…huyu ni jungu kuu…” @Neema Ruth akaeleza.

“Waah! Miaka 30 ni wachumba waliofanikisha ndoa. Hongera,” akapongeza @Jane Mwaura.

Wengine kama @Masesi Wa Kalulu walizua utani kutokana na ucheshi wake wakati akiigiza katika Makala ya Vioja Mahakamani. “Hapa unajitetea ukiwa upande gani?” Masesi akazua ucheshi.

“Ukiwa upande huu hautaapishwa na hautaulizwa maswali,” akaongeza @Bernard Kamau Alex.

Waasisi wa Thriving Couples KE wamejitambua kama Keith Dindi na Esther.

“Esther na mimi tulianzisha kundi hili kwa sababu tunaamini ahadi ya upendo. Nilimuomba posa miaka 20 iliyopita, tulikuwa wadogo kiumri na upendo ulinoga. Hatukuwa na chochote tulipoanza safari ya ndoa, ila ukosefu wa pesa haukuwa kizingiti kuanzisha familia. Pesa haziwezi kununua upendo,” Keith Dindi anaelezea kwenye mojawapo ya chapisho linaloandamana na picha zao.

Kulingana na mwasisi huyo, hadithi ya safari yao kwenye ndoa licha ya changamoto walizopitia, ni kielelezo au mfano wa wanandoa wawe na matumaini.

“Tunajifafanua kama nguzo ya matumaini, na ndilo lengo la kundi hili. Kurejesha matumaini na kuwapa watu motisha kuwa na imani na ndoa. Tubadilishe mawazo potovu yanayosambaratisha ndoa, ndoa ni tamu, unaweza kufanikisha uhusiano, tukumbatie ndoa na tuifurahie. Wanaume wawe waaminifu na wake wawe watiifu, tufanikiwe pamoja…” @Keith anaendelea kufafanua.

Akishukuru kwa dhati wanaoridhia kundi hilo, Keith hata hivyo anasema safari kuliimarisha haijakuwa rahisi kwani kuna wanaokosoa msimamo wao kuhusu ndoa.

Anahimiza wachangiaji kufanya kundi hilo kuwa sauti moja ya mamilioni ya wanandoa kuimarisha ndoa na uhusiano.

  • Tags

You can share this post!

Limbukeni Kiprop na Chirchir watamalaki Mbio za Nyika za AK...

Vikosi vya raga ya Kenya Cup vyakumbatia mfumo wa mechi za...