Vijana wamzuia Gideon kupokea baraka

ONYANGO K’ONYANGO na TOM MATOKE

KIZAAZAA kilitokea katika eneo la Kapsisiywa kaunti ya Nandi jana alfajiri wakati vijana walimzuia Seneta wa Baringo Gedion Moi aliye pia mwenyekiti wa KANU kufanya mkutano.

Inasemekana Bw Moi aliwasili katika eneo hilo kati ya saa 10 na saa 12 alfajiri lakini vijana waliokuwa na hamaki na hasira kali wakamzuia akienda nyumbani kwa naibu wa mwenyekiti wa baraza la wazee wa jamii ya Talai aliyeondolewa mamlakani Bw Christopher Koyogi kumtawaza kuwa kiongozi wa jamii ya Wakalenjin.

Vijana hao wanaomuunga mkono naibu wa Rais Dkt William Ruto walitumia taya (magurudumu), magogo na mawe kuziba barabara ya Chepterit-Baraton-Sang’alo karibu na Kimondi. Barabara hii inaelekea nyumbani kwa Mzee Koyogi.

Vijana hawa walimkashfu Seneta Moi na Bw Koyogi kwa kukaidi utamaduni wa Talai kuhusu utawazaji wa viongozi.

Vijana hao waliokuwa na hamaki waliambia TaifaLeo kuwa Bw Moi alijaribu kuingia nyumbani kwa Bw Koyogi karibu na shule ya msingi ya Kapsisiywa alfajiri na mapema lakini wakatifua azma yake.

“Mwendo wa saa mbili na saa tatu usiku mnamo Ijumaa tulipashwa habari kuwa kuna mgeni maalum ambaye angelitembelea eneo hilo kwa mwaliko wa Wazee ndipo tukagundua ni Seneta Moi aliyetazamia kutawazwa ndipo tukajipanga na kumzuia,” alisema mmoja wa vijana hao Bw William Serem.

“Msafara wake wa magari ulijaribu kuingia kwa Bw Koyogi kati ya saa 10 na saa 11 alfajiri katika barabara ya Kabiyet -Sang’alo lakini tukaiziba barabara hiyo kwa vile hatungeruhusu utawazaji mwingine kufanyika,” alisema Bw Lenix Rono, mwanarika mwingine.

Walishangaa sababu ya mwana huyo wa hayati Daniel Toroitich Arap Moi kutoandamana na viongozi kama vile Gavana Stephen Sang.

“Hatutawakubalia baadhi ya Wazee wa jamii ya Talai kugeuza utawazaji kuwa biashara,” alisema Bw Elijah Murei.

Vijana hao walimtaka Bw Moi awahutubie na kueleza msimamo wake kuhusu azma ya Dkt Ruto kuwania urais 2022 lakini akahepa suala hilo.

Duru zasema kuwa Seneta Moi aliwabembeleza vijana hao wamruhusu aingie nyumbani kwa Bw Koyogi kwa vile ni mwana wa hayati Daniel arap Moi aliyeheshimiwa na kupendwa na Wakalenjin wote lakini wakakataa.

Kwa mujibu wa baraza la Wazee wa Jamii ya Talai, Kasisi James Bassy, tamaduni haziruhusu utawazaji mwingine kufanywa.

“Katika tamaduni zetu hatuwezi kuruhusu utawazaji mwingine kufanyika mbali na ule wa Dkt Ruto wa mwaka uliopita,”alisema Bw Bassy.

“Ndio Bw Moi alijaribu kuingia hapa akitazamia kutawazwa na mwenzetu anayejulikana kwa jina Koyogi aliyepinga kutawazwa kwa Dkt Ruto,” alisema Mzee Amos Korir mmoja wa baraza la wazee wa Talai, aliyeongeza, “Hatungeruhusu jambo hilo kufanyika ndipo tukawaambia vijana wamzuie kuingia kwa mwenzetu Koyogi.”

Mng’ang’ano wa atakayekuwa kiongozi wa jamii ya Wakalenjin umejitokeza wazi kati ya Bw Moi na Dkt Ruto.

Kila mmoja ya wawili hao anataka ubambe wa eneo hilo la Rift Valley lililo na idadi kubwa ya wapiga kura nchini kabla ya uchaguzi mkuu wa 2021.

Kati yao hakuna aliyelemaa kifedha na wataonana ana kwa ana katika harakati za atakayekuwa kinara wa Rift Valley.

Kumekuwa na mkinzano mkali kati ya Bw Moi na naibu huyu wa Rais katika siku za hivi punde huku kila mmoja akijaribu kumtoa manyoya mwenzake katika harakati za kuthibiti eneo hilo linalotambulika kuwqa ghala kuu la kura.

Kwa muda wa miaka 10 iliyopita Dkt Ruto amekuwa akifurahia umiliki wa masuala ya kisiasa na kumsukuma Bw Moi pembeni lakini wimbi la siasa za kitaifa linalovumishwa na Rais Uhuru Kenyatta limebadili mambo.

Sasa Bw Moi yuko na umaarufu mwingi Rift Valley.

Washauri wa kisiasa waliokuwa na hayati Moi wamejitosa ulingoni kumpigia debe seneta huyo katika kidumbwedumbwe cha urais 2022.

Dkt Ruto na washauri wake wamevurugika na kuingia kwa kasi kwa Bw Moi katika siasa za Rift Valley huku wakiwatumia wawakilishi wa wadi na wazee kumzuia seneta huyo kuwafikia wananchi.