• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
Cotu yapinga kuongezwa kwa ushuru wa mapato

Cotu yapinga kuongezwa kwa ushuru wa mapato

Na IBRAHIM ORUKO

MUUNGANO wa vyama vya kutetea haki za wafanyakazi (COTU) umeishutumu serikali kwa kuongeza kwa asilimia 30 kodi inayotozwa wafanyakazi wanaopokea mishahara kuanzia 32,333.

COTU imeitaka Wizara ya Fedha itafute njia mbadala za kupata fedha za kuendeleza uchumi badala ya kuwalimbikizia kodi ya ziada wafanyakazi ambao tayari wanalemewa na mzigo wa kodi.

COTU pia imeishauri mamlaka ya kukusanya ushuru nchini (KRA) ibuni mikakati mipya ya kuwaandama Wakenya ambao hukwepa kulipa kodi.

Muungano huu wa vyama ulisema ni jambo la aibu kwa KRA kuwatoza wafanyakazi viwango vya juu vya kodi na tayari wameathiriwa zaidi na makali ya mkurupuko wa ugonjwa wa Covid-19.

Katibu Mkuu wa muungano huo nchini Francis Atwoli alisema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari kuwa, Serikali haipasi kuwatoza wafanyakazi kodi zaidi kwa vile wanaendelea kuumia kutokana na janga la ugonjwa wa Corona ulioathiri sekta zote za uchumi.

“Wizara ya Fedha inastahili kuuwianisha utoaji huduma kwa wananchi na kuwabebesha mzigo wa ulipaji kodi ya juu,” alisema Bw Atwoli katika taarifa aliyotoa kwa wanahabari.

Katibu huyo alitoa taarifa hiyo kufuatia ufichuzi Alhamisi wiki hii katika habari zilizochapishwa katika magazeti ya Taifa/Nation kwamba, serikali itawatoza wafanyakazi wanaopokea mshahara wa Sh32,333 kodi ya asilimia 30.

Bw Atwoli alisema Cotu inapinga vikali uamuzi huo na kuikumbusha Serikali kuwa wafanyakazi wameathiriwa pakubwa na janga hilo. Alisema wengi wa wafanyakazi wanahangaika kupata chakula.

Katika sheria iliyopitishwa wiki iliyopita Bunge lilifutilia mbali afueni ya kupunguza ulipaji ada iliyotangazwa na Serikali mwaka 2020 corona ilipokita mizizi.

  • Tags

You can share this post!

Maandalizi duni shule zikifunguliwa kesho

Mbunge ashutumu Rais kuporomosha uchumi