• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Mbunge ashutumu Rais kuporomosha uchumi

Mbunge ashutumu Rais kuporomosha uchumi

Na CHARLES LWANGA

MBUNGE wa Kandara, Bi Alice Wahome, amemtaka Rais Uhuru Kenyatta akubali kuwa hali ngumu ya maisha wanayopitia Wakenya ameisababisha mwenyewe na wandani wake wa karibu.

Akihutubia wanahabari katika hoteli ya Sea View mjini Malindi, Bi Wahome alisema kubadilisha Katiba kamwe si suluhu kwa matatizo ya kiuchumi yanayoikumba nchi kwa sasa.

“Uchumi wetu umo hatarini. Kuna ukosefu wa ajira na hali ngumu ya maisha. Benki zinashirikiana na serikali kumkandamiza raia wenye mapato ya chini. Masomo ya watoto wetu yako hatarini. Serikali za kaunti hazipokei fedha kwa wakati unaofaa, na ugatuzi umesambaratika huku huduma muhimu zikiwa karibu kufungwa,” akasema.

Mbunge huyo alionya kwamba Wakenya watajuta ikiwa watamkubali Bw Kenyatta kupitia kwa Bw Raila Odinga, kubadilisha Katiba ya Kenya 2010 kama angali uongozini.

“Hatua ya Rais Kenyatta kujaribu kubadilisha katiba ni usaliti mkubwa kwa Wakenya na katiba ambayo aliapa kuilinda. Sasa anatumia ujanja kubadilisha Katiba kinyume na matakwa ya Wakenya ili asalie uongozini hata akiwa amestaafu baada ya uchaguzi mkuu wa 2022,” akasema.

Alimtaka Rais Kenyatta akubali kwamba ameporomosha uchumi wa nchi kutokana na sera mbovu za kiuchumi alizozipendekeza katika miaka yake saba ya uongozi.

Bi Wahome alisema idara za haki kama kitengo huru pia zimekandamizwa na serikali kwa kupunguziwa bajeti.

Mwandani huyo wa Naibu Rais, Dkt William Ruto kupitia mrengo wa ‘Tangatanga’, alisema Rais Kenyatta amedharau na kupuuza kutekelezwa kwa Katiba ya Kenya ya 2010.

  • Tags

You can share this post!

Cotu yapinga kuongezwa kwa ushuru wa mapato

JAMVI: Mwamko wa Ruto Pwani ni mwisho wa Raila, Joho?