• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
JAMVI: Mwamko wa Ruto Pwani ni mwisho wa Raila, Joho?

JAMVI: Mwamko wa Ruto Pwani ni mwisho wa Raila, Joho?

Na WANDERI KAMAU

KIVUMBI cha udhibiti wa siasa za Pwani kilianza rasmi Alhamisi ielekeapo 2022, baada ya wabunge wa ‘Tangatanga’ kutangaza vita vikali vya kisiasa dhidi kinara wa ODM Raila Odinga na washirika wake katika ukanda huo.

Miongoni mwa wale wanaoonekana kulengwa zaidi kwenye ‘vita’ hivyo ni Gavana Hassan Joho wa Mombasa, maarufu kama ‘Sultan’, ambaye amekuwa akionekana kama mfalme wa siasa za Pwani.

Wabunge hao walitoa kauli hizo kwenye hafla ya kusherehekea ushindi wa mbunge mpya wa eneo la Msambweni, Feisal Bader, aliyewania kama mgombea huru kwa kuungwa mkono na Naibu Rais William Ruto.

Ni hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Dkt Ruto na zaidi ya wabunge 30 wa mrengo huo.

Bader alitangazwa mshindi kwenye uchaguzi huo uliofanyika Desemba 15 kwa kupata kura 15, 251 dhidi ya Bw Omar Boga, aliyewania kwa tiketi ya ODM ambaye alizoa kura 10,444.

Ni ushindi ambao umeonekana kuzua msisimko wa aina yake katika kundi la ‘Tangatanga’ ambapo sasa limedai matokeo hayo ni taswira kamili kwamba Bw Odinga hana ushawishi wowote kisiasa katika ukanda huo.

Miongoni mwa viongozi waliotoa matamshi makali ni Aisha Jumwa (Malindi), Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Benjamin Tayari (Kinango), Gavana Salim Mvurya (Kwale) kati wanasiasa wengine.

Akionekana mwenye hisia, Bi Jumwa alitaja ushindi huo kama ishara kamili kwamba “Wapwani wameanza safari ya kujikomboa kutoka siasa za kibepari.”

“Mpwani amedhihirisha wazi hatashurutishwa kufanya maamuzi ya kisiasa mkwa nguvu. Ushindi huu umeonyesha Wapwani wameamua kufanya maamuzi yao kwa njia huru kwa kuwachagua viongozi wanaowapenda wenyewe. Huu ni mwanzo wa ukombozi,” akasema Bi Jumwa.

Kauli yake iliungwa mkono na Bw Mwashetani, aliyesema “wageni” hawana tena usemi kuhusu mwelekeo wa siasa za Pwani.

Bw Mvurya naye alisema mwelekeo huo unaashiria wenyeji wa eneo hilo wameanza kuonyesha imani na uongozi na utendakazi wa Dkt Ruto.

Ikizingatiwa walitoa matamshi hayo mbele ya Dkt Ruto, wadadisi wa siasa wanasema kuwa uchaguzi huo ulikuwa muhimu sana, kwani kuna chaguzi zingine ndogo ambazo ushindani kama huo unatarajiwa kushuhudiwa.

Chaguzi hizo zimepangiwa kufanyika katika maeneobunge ya Matungu na Kabuchai katika kaunti za Kakamega na Bungoma mtawalia. Hilo ni kufuatia vifo vya wabunge Justus Murunga na James Lusweti.

Uchaguzi mwingine pia umepangiwa kufanyika katika Kaunti ya Machakos mnamo Machi, kufuatia kifo cha Seneta Boniface Kabaka.

“Kabla ya uchaguzi huo kufanyika, Bw Odinga alisema matokeo yake yangeonyesha taswira kamili kuhusu ikiwa Wakenya wanaunga mkono ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) au la. Ukweli ni kuwa ODM inakabiliwa na uhalisia mchungu kuwa hali si shwari hata kidogo kama ilivyokuwa awali. Uhalisia huo ni mpana kushinda uhifadhi wa kiti hicho pekee,” asema Bw Charles Mulila, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za Pwani.

Mnamo Jumatano, Bw Odinga alifanya kikao na viongozi wa chama walioongoza kampeni hizo katika hoteli moja Kaunti ya Kilifi.

Duru katika mkutano huo zilisema ulikumbwa na majibizano, huku viongozi wakilaumiana wao kwa wao kwa kutoshirikiana ifaavyo kwenye kampeni hizo.

Kwa mujibu wa baadhi ya viongozi waliohudhuria, sababu zilizotajwa kuchangia kushindwa kwao ni ukosefu wa ushirikiano baina ya viongozi, ukosefu wa fedha za kutosha huku baadhi ya viongozi wakidaiwa kumuunga mkono Feisal kisiri.

Licha ya matatizo hayo, Bw Odinga alipuuzilia mbali dhana kwamba chama hicho kimeanza kupoteza umaarufu wake Pwani.

“ODM ingali imara. Tumebaini sababu kadhaa ambazo zilichangia matokeo hayo, ila hatuwezi kuziweka hadharani kwa sasa,” akasema.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni Bw Joho, mbunge Junet Mohamed (Suna Mashariki) ambaye pia ndiye Mkurugenzi wa Chaguzi, mwenyekiti wa ODM tawi la Kwale Hassan Mwanyoha, Sheikh Juma Ngao kati ya wengine.

Kama Bw Odinga, Bw Mohamed alisema licha ya ushindi huo, ‘Tangatanga’ haina utambulisho maalum wa kisiasa nchini, hivyo hilo haliwezi kuwapa wasiwasi hata kidogo.

“Haijulikani upande ambao ‘Tangatanga’ wanaegemea kisiasa; haifahamiki ikiwa wako serikalini au upinzani. Hivyo, hilo haliwezi kutushtua hata kidogo,” akasema Junet.

Licha ya kauli hizo, wadadisi wanasema matokeo hayo yamewapa usemi na mwamko mpya kisiasa viongozi waasi kama Jumwa, mbunge Mohamed Ali (Nyali) kati ya wengine, kwani Bw Joho amekuwa akionekana kuwa msemaji wa kisiasa katika ukanda huo.

“Hilo ni pigo kubwa kwa Joho, kwani imedaiwa analenga kuhudumu kama mojawapo ya manaibu wawili wa Waziri Mkuu, ikiwa Wakenya wataipitisha ripoti ya BBI. Hilo pia ni ishara ya hatari kwa nia ya Bw Odinga kisiasa, ikiwa atawania urais 2022,” akasema Prof Edward Kisiang’ani, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Hata hivyo, wanasema ni mapema sana kwa Dkt Ruto na kundi la ‘Tangatanga’ kupumbazwa na ushindi huo, kwani hali inaweza kubadilika, ikizingatiwa Bw Joho bado ana ushawishi wa kisiasa na kifedha.

You can share this post!

Mbunge ashutumu Rais kuporomosha uchumi

Maskini jeuri?