• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
JAMVI: Uhuru alivyosagasaga Sonko, Waititu kisiasa

JAMVI: Uhuru alivyosagasaga Sonko, Waititu kisiasa

Na BENSON MATHEKA

IKIWA kuna jambo ambalo waliokuwa magavana Mike Sonko (Nairobi) na Ferdinard Waititu (Kiambu) hawatasahau katika maisha yao, ni jinsi Rais Uhuru Kenyatta alivyochangia kutia kikomo maisha yao ya uongozi.

Wawili hao waliondolewa ofisini kwa madai ya ufisadi na kutumia vibaya mamlaka yao na kulingana na mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Bw Wafula Chebukati, hawawezi kugombea kiti chochote cha uongozi au kushikilia wadhifa wowote wa umma.

Hivi ndivyo inavyosema katiba kumaanisha kwamba wawili hao wanaweza tu kushiriki siasa bila kugombea viti vya uongozi.

Wawili hao walijipata pabaya baada ya kutofautiana na Rais Kenyatta na washirika wake wa kisiasa kwa kumuunga Naibu Rais William Ruto kumpinga handisheki kati ya kiongozi wa nchi na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.

“Madai ya ufisadi ni mahakama inayofaa kuamua iwapo wako na hatia lakini shinikizo ziliwekwa madiwani wakawatimua kwa kuwa hawakutakiwa na kiongozi wa nchi kwa kumpinga na kuelekeza uaminifu wao kwingine. Hii haikutendeka kwa magavana wengine ambao wanakabiliwa na kesi sawa, kwa sababu wawili hao walichukuliwa kuwa na madharau na umuhimu wa kaunti zao,” asema mdadisi wa siasa John Koech.

Bw Waititu ambaye alikuwa wa kwanza kuondolewa ofisini alijikaanga kwa kutofautiana na viongozi wa Kaunti ya Kiambu akiwemo Rais Kenyatta.

“Bw Waititu alisahau kwamba alikuwa gavana wa kaunti ya nyumbani ya Rais ambaye hangekubali uongozi mbaya na matumizi ya pesa yanayotiliwa shaka ilhali anasisitiza ufisadi ukomeshwe kisha akajipiga kifua kupinga BBI. Kwa kufanya hivi, alijichimbia kaburi kisiasa,” alisema Bw Koech.

Hali sawa ilimpata Bw Sonko ambaye alisahau kwamba jiji la Nairobi ni makao makuu ya serikali na kitovu cha biashara Afrika Mashariki. Alianza kupiga vita maafisa wa serikali waliokuwa wakiwakilisha maslahi ya wenye ushawishi na akakataa kumtii Rais Kenyatta licha ya awali kumsaidia asibanduliwe na madiwani kwa kuhamishia baadhi ya majukumu kwa serikali kuu.

TIKETI

Wadadisi wa siasa wanasema kile ambacho Bw Sonko na Bw Waititu walisahau ni kwamba walipata tiketi za chama cha Jubilee kugombea viti vya ugavana kinyume na mapenzi ya Rais Kenyatta na washirika wake wa kisiasa.

“Ilikuwa wazi kwamba wawili hao walikuwa miongoni mwa watu ambao Naibu Rais William Ruto alihakikisha walipata tiketi za Jubilee ili kulinda maslahi yake. Badala ya kuchanuka na kuegemea upande wa handisheki waliposhinda walianza kupinga BBI wakasahau ni nani anayeongoza nchi,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

“Angalia mtindo uliotumiwa kuwaondoa mamlakani. Ilianza kwa kutofautiana na manaibu wao, kisha wakavurugana na madiwani, wakashtakiwa kwa makosa ya ufisadi na kutumia vibaya ofisi zao na kuondolewa kupitia vikao vya maseneta wote na hatua hiyo kuchapishwa mara moja katika ilani spesheli ya gazeti rasmi la serikali. Mbona Gavana Waiguru hakusikilizwa na kikao kama hicho mbali na kamati ya seneti?” ahoji Bw Kamwanah.

Bw Waititu alitofautiana na naibu wake James Nyoro(aliyemrithi) naye Bw Sonko alitofautiana na Polycarp Igathe aliyejiuzulu.

Kulingana na wadadisi, wawili hao hawakufahamu uzito wa kuondolewa ofisini hadi juzi, Bw Waititu alipomezea mate kiti kilichoachwa wazi na Bw Sonko kaunti ya Nairobi kama mgombea huru.

Bw Chebukati aliweka wazi kuwa tume yake haiwezi kumuidhinisha mtu aliyeondolewa ofisini kupitia mswada wa kumtimua kugombea kiti chochote. Wakili Otiende Amollo mmoja wa wataalamu walioandika katiba ya 2010, alikubaliana na Bw Chebukati kwamba Bw Waititu hawezi kushiriki uchaguzi wowote.

“Tulipoandika katiba kufafanua kwamba mtu akiondolewa ofisini kwa sababu ya matumizi mabaya ya pesa, tulinuia kuzuia watu waliopatikana na hatia ya kutumia uchaguzi kurejea mamlakani tena,” alisema Bw Amollo. Inasemekana Bw Sonko anamezea mate kiti kwenye uchaguzi mkuu ujao na amewasilisha kesi kortini kupinga mfumo wa kuondolewa kwake.

Lakini kulingana na Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki ambaye ni mtaalamu wa katiba, magavana wanaoondolewa ofisini kupitia mswada wa kuwatimua hawawezi kugombea kiti chochote katika uchaguzi au kushikilia wadhifa wowote wa umma nchini Kenya.

Kindiki anasema kwamba masuala ya matumizi mabaya ya ofisini ni ya kimaadili na ukiukaji wa sura ya sita ya katiba. “ Katiba inamzima mtu anayeondolewa ofisini kwa sababu ya kukiuka maadili kugombea kiti chochote au kushikilia wadhifa wa umma nchini Kenya,” asema.

You can share this post!

Maskini jeuri?

JAMVI: Mikosi ya usaliti kwa miungano ya kisiasa uchaguzi...