• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Guardiola kuwa kocha kwa muda mrefu zaidi kuliko jinsi alivyotarajia hapo awali

Guardiola kuwa kocha kwa muda mrefu zaidi kuliko jinsi alivyotarajia hapo awali

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City amesema huenda akasalia katika ulingo wa ukufunzi wa soka kwa muda mrefu zaidi kuliko jinsi alivyotarajia hapo awali.

Guardiola, 49, aliwahi kufichua azma ya kustaafu mapema kitaaluma ili kujitosa katika ‘masuala mengine tofauti’.

“Awali, nilidhani ningejiondoa katika ulingo wa soka mapema kama nilivyokuwa nimepanga. Sasa sioni uwezekano wa hayo kutimia na huenda nikalazimika kusukuma gurudumu hili la ukufunzi hadi uzeeni. Hivyo, sijui itakuwaje,” akasema kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich.

Mnamo Novemba, Guardiola ambaye ni raia wa Uhispania, alitia saini mkataba mpya na Man-City ambao amewashindia mataji sita tangu atie guu ugani Etihad mwanzoni mwa msimu wa 2016-17.

Hadi alipokubali kudhibiti mikoba ya Man-City, Guardiola ambaye atafikisha umri wa miaka 50 mwezi huu, alikuwa amehudumu Barcelona kwa miaka minne kabla ya kuwatia makali masogora wa Bayern nchini Ujerumani kwa miaka mitatu.

“Tajriba ni jambo muhimu sana katika ukufunzi. Kadri unavyosalia katika taaluma, ndivyo kazi hii inakuwa ya kuvutia hata zaidi. Changamoto zinakuwa nyingi na ubunifu wa kuzikabili unaimarika pia,” akaongeza kocha huyo aliyewahi kuhusishwa na uwezekano wa kuhamia Juventus ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) baada ya kuagana na Man-City.

Kwa kutia saini kandarasi mpya ugani Etihad, Guardiola alijipa uhakika wa kuhudumu kambini mwa Man-City kwa miaka mitano, huu ukiwa muda mrefu zaidi ambao amewahi kuhudumu katika kikosi kimoja akiwa kocha.

Tangu 2016, amewaongoza waajiri wake kutia kibindoni mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Kombe la FA na mataji matatu ya League Cup. Kufikia sasa, kikosi chake bado kinafukuzia mataji manne yakiwemo Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), EPL, FA na Carabao Cup.

Baada ya kuvaana na Chelsea katika EPL mnamo Januari 3, 2020, Man-City watashuka dimbani kupepetana na Manchester United katika nusu-fainali za Carabao Cup mnamo Januari 6 ugani Old Trafford.

You can share this post!

TAHARIRI: Msimamo wa Cotu ni machozi ya mamba

DINI: ‘Sijambo’ neno la kufungua mwaka na...