• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
DINI: ‘Sijambo’ neno la kufungua mwaka na kuhesabu baraka badala ya balaa

DINI: ‘Sijambo’ neno la kufungua mwaka na kuhesabu baraka badala ya balaa

Na FAUSTIN KAMUGISHA

TUNAPOFUNGUA mwaka mpya wa 2021, wengi tutalitamka neno sijambo.

Unapofungua siku unaweza kutamka neno sijambo. Paka akipigwa teke akaangukia kwenye bakuli ya maziwa bila shaka atasema, sijambo. Unaposema, sijambo unaegemea upande mzuri wa mambo. Neno sijambo ni kuhesabu baraka badala ya balaa. “Dunia inategemea matokeo. Usiwaambie wengine kuhusu uchungu wa kuzaa. Waonyeshe mtoto!” alisema Arnold Glasow.

Mama aliyejifungua mtoto anaposalimiwa: hujambo akajibu sijambo si kwamba, hakuona uchungu wa kuzaa. Neno sijambo linabainisha mtazamo chanya. Licha ya machungu, kuna mtoto. Licha ya miiba katika mawaridi, kuna maua. Wahaya wanapompongeza mama aliyejifungua mtoto wanamwambia, “Rudi tena hakuna miiba.” Wanafunika uchungu wa kuzaa na kubeba mimba, wanatazama maua ya kuzaliwa mtoto. Mnapofungua mwaka 2021 nawasalimia, hamjambo! Bila shaka mtanijibu: Hatujambo! Neno , hatujambo linafunika huzuni, misiba, sononeko, machungu, hisia mbaya, hasara, machozi, mateso na kupoteza.

Neno sijambo ni neno la kuomba muujiza; kwamba pasiwepo jambo baya au tukio baya. Miujiza ipo mdomoni. Neno sijambo ni ombi la Mungu apishe mbali jambo baya. Mungu arekebishe. Muumba ahuishe. Neno linaumba. Nabii Elisha alimtuma mtumishi wake Gehazi akutane na mwanamke Mshunami mwenye uchungu moyoni. Alimwambia: “Tazama, Mshunani yule anakuja! Basi, nenda upesi kumlaki, ukamuulize, haujambo? Mumeo hajambo? Mwanao hajambo? Mwanamke akajibu: “Hatujambo!” (2 Wafalme 4: 25-26). Mwanamke aliyesema: “Hatujambo!” tunaambiwa “roho yake imejaa uchungu.” Baada ya maombezi ya nabii Elisha tunaambiwa, “mtoto akapiga chafya mara saba, na mtoto akafumbua macho yake” (2 Wafalme 4: 25-26). Kweli neno hatujambo linaumba. “Maneno ni magari yanayoweza kutusafirisha kutoka kwenye mchanga usiovutia mpaka kwenye nyota zinazomeremeta,” alisema M. Robert Southey. Maneno tuyatumie kwa uangalifu mkubwa.

Kuna mume na mke ambao walikuwa wezi. Wakati mke akiwa na mimba walisema, mtoto atakayezaliwa awe mwizi kama yeye. Muda mfupi mtoto alipozaliwa, mkunga alilalamika kuwa haoni pete yake. Walipokunjua mkono wa mtoto waliikuta pete ya mkunga. Mtoto aliisha anza kazi. Hadithi hiyo inatupa somo la kutumia maneno kwa uangalifu. Maneno yanaumba.

Neno sijambo linaakisi mtazamo chanya, licha ya shida au mateso, kuna mazuri. Kuna mwanaume aliyepoteza mguu katika ajali aliposaidiwa kupelekwa hospitalini aligundua kuwa amepoteza mguu. Aliwaambia waliomzunguka na kumuuliza, hujambo, “Sijambo, namshukuru Mungu nimepoteza mguu wenye ugonjwa wa baridi yabisi.” Alikuwa na mtazamo chanya. Mwenye mtazamo hasi anasema mvua itasababisha matope, mwenye mtazamo chanya anasema, mvua itatuliza vumbi. Mwenye mtazamo hasi akiona maua aina ya waridi anasema, maua yana miiba. Lakini mwenye mtazamo chanya akiona maua aina ya waridi anasema, miiba ina maua. Mwenye mtazamo chanya anasema, leo niko vizuri, sijambo. Mwenye mtazamo hasi anasema jana sikuhisi visuri nilikuwa na mambo mabaya. Mwenye mtazamo chanya anasema, namshukuru Mungu niko hai.

Mwenye mtazamo hasi anasema, nasikitika ipo siku nitakufa. Mwenye mtazamo chanya anaona fursa katika kila changamoto. Mwenye mtazamo hasi anaona changamoto katika kila fursa.

Neno sijambo ni sala. Mojawapo ya mafundisho makubwa ya Biblia ni kuwa, Mungu anajibu sala. Alijibu sala ya sijambo ya mwanamke Mshunami aliyepoteza mtoto wake. Sala ya sijambo ipae mbinguni kama moshi wa ubani altareni. Sala na matendo viiambatane pamoja. Unaposema sijambo, fanya liwezekanalo pasiwepo na jambo baya na pasiwepo na figisufigisu. Kuna baba aliyekuwa anaongoza sala za familia. Alimuomba Mungu amtazame kwa jicho la huruma mjane maskini jirani yao. Machozi ya huruma yalitiririka kwenye shavu la mke wake.

Lakini mtoto kifungua mimba hakuwa anasali. Baba yake aliposema, amina alimwendea na kumwambia, baba nipe pochi yako nitamwendea maskini huyo nakujibu sala yako mimi mwenyewe. Shiriki majibu ya sala.

Wahaya wa Bukoba nchini Tanzania wana utararibu wa kuita mwaka jina. Mwaka huu 2021 umeitwa BAGARA (PALILIA). Ukimuomba Mungu mavuno palilia shamba. Shiriki majibu ya sala. “Palilia” biashara. “Palilia” mpango au mkakati wako. “Palilia” ndoa yako. Yafanyie kazi maneno SIJAMBO NA HATUJAMBO. Kufunga mwaka ni kufunga mahesabu na kufungua mahesabu. Mali bila daftari hupotea bila habari. Unaposema sijambo, funga na kufungua mahesabu.

You can share this post!

Guardiola kuwa kocha kwa muda mrefu zaidi kuliko jinsi...

Mke akaangwa kutema mume aliyefutwa