Mke akaangwa kutema mume aliyefutwa

Na CORNELIUS MUTISYA

KAVIANI, MACHAKOS

MAMA wa hapa alizomewa vikali na wenzake kwa kumpuuza mumewe alipofutwa kazi na kuanza kumezea mate waume wa wanawake wengine.

Kulingana na mdokezi, mama huyo aliolewa yapata miaka sita iliyopita kwenye harusi ya kikristo. Mumewe alikuwa anachapa kazi jijini Nairobi na alikuwa akipokea mshahara mnono. Walijaliwa watoto wawili wa kiume na walikuwa wakiishi bila vurugu.

Hata hivyo, uhusiano wao mzuri ulianza kudorora mara tu, mumewe aliposimamishwa kazini mwaka jana na akarejea nyumbani.

“Jamaa alikumbatia kikamilifu busara ya wahenga kuwa ng’ombe akivunjika guu malishoni hurudi zizini kusaidiwa. Alirejea nyumbani ili ajaribu bahati yake katika fani zingine za maisha,’’ alisema mpambe wetu.

Inaarifiwa kuwa, alikosa pesa za kumpodoa mkewe kama ilivyokuwa kawaida yake akiwa kazini na uhusiano wao ukaanza kufifia na kupoteza ladha kabisa.

Ripoti za mtaa zaarifu kuwa, mkewe alianza kumea pembe mpaka akawa kichwa ngumu. Alianza kumchafulia mumewe jina kwa wanaume wengine mitaani huku akiwatongoza.

Inasemekana kwamba, tabia yake iliwakera mno wanawake wengine mpaka wakakata kauli kumzima ili awe funzo kwa wanaonyemelea waume wa wenyewe.

“Umeshindwa kabisa kumtunza mumeo ndipo unyemelee wale wetu? Usipokoma, tutakuonyesha kilichomtoa kanga manyoya shingoni,’’ mama mmoja alifoka kwa hasira.

Duru zaarifu kuwa, mama huyo alizomewa vikali na akaamua kuomba msamaha. Alisamehewa na akaonywa dhidi ya kuwa na jicho la nje huku akishauriwa kumheshimu mumewe hata kama hana kazi.

“Baada ya kisa hicho, mama huyo alibadili tabia na kuanza kumheshimu mumewe,’’ asema mdaku wetu.