• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:55 AM
Wenger asema ‘niko tayari kurejea Arsenal kuokoa jahazi’

Wenger asema ‘niko tayari kurejea Arsenal kuokoa jahazi’

Na MASHIRIKA

ARSENE Wenger amesema kwamba atakuwa radhi kurejea uwanjani Emirates kumsaidia kocha Mikel Arteta kurejeshea miamba uthabiti waliojivunia hapo zamani iwapo usimamizi utamwomba kumfanya hivyo.

Isitoshe, Wenger amefichua kwamba atahiari kurudi Emirates ‘kuokoa jahazi’ iwapo Arsenal watazama tena jinsi hali ilivyokuwa katika mechi saba za awali kabla ya Arteta kuongoza ufufuo wa kikosi hicho dhidi ya Chelsea kwa ushindi wa 3-1 mnamo Disemba 26, 2020.

Tangu wakati huo, Arsenal wamesajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Brighton na mwingine wa 4-0 dhidi ya West Bromwich Albion.

Ingawa hivyo, mwanzo mbaya katika kampeni za EPL msimu huu chini ya Arteta aliyeajiriwa Disemba 2019, umewadumisha Arsenal chini ya mduara wa vikosi 10 vya kwanza na kwa sasa wanashikilia nafasi ya 11 kwa alama 23 baada ya mechi 17.

Wenger alihudumu kambini mwa Arsenal kwa miaka 22 kabla ya kuagana na kikosi hicho mwishoni mwa msimu wa 2017-18.

“Iwapo nitahitajika, nitarudi ili nimsaidie Arteta kufanya kazi. Japo sitarajii hilo kufanyika kwa sasa kwa sababu kikosi kimeanza kujinyanyua. Lakini kikiyumba tena na nione dalili za kuzama kwa jahazi, nitafanya hima na kwenda kukoa bila ya kusubiri kuambiwa,” akasema Wenger, 71.

Awali, Wenger alisema kwamba Arteta ana ‘bahati kubwa’ ya ‘kuangukia’ kazi ya ukocha katika klabu ‘kubwa’ licha ya kukosa tajriba pana na uzoefu wa kutosha katika ulingo wa ukufunzi.

“Ana bahati ya mtende kupata kazi ya ukufunzi katika kikosi cha Arsenal muda mfupi tu baada ya kuangika daluga zake za usogora. Kikawaida, mtu huhitaji zaidi ya miaka 10 ya ukufunzi katika vikosi vya hadhi ya chini kabla ya kupanda ngazi na kufikia aliko Arteta kwa sasa,” akasema kocha huyo raia wa Ufaransa.

“Lakini kwa sababu alichezea Arenal na alikuwa mchezaji mzuri mwenye sifa za uongozi na nidhamu tele, basi milango ya heri ilimfungukia kirahisi na ninamtakia kila la heri,” akaongeza.

Kabla ya kuajiriwa na Shirikisho la Soka Duniani kusimamia masuala ya makuzi na maendeleo ya kabumbu ulimwenguni, Wenger alipokezwa ofa tele za ukufunzi kambini mwa Barcelona, Galatasaray, Real Madrid, PSG, Fulham na timu za taifa za Qatar, Uholanzi na Ufaransa.

You can share this post!

SHULE: Wadau muhimu ngazi zote za serikali waelezea...

Serikali yabuni kituo cha kufuatilia habari kuhusu visa vya...