Serikali yabuni kituo cha kufuatilia habari kuhusu visa vya Covid-19 baada ya shule kufunguliwa

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI kwa ushirikiano na wadau katika sekta ya elimu, imeweka mikakati ya pamoja ya kufanikisha ufunguzi wa shule kuanzia Jumatatu, Januari 4, 2020.

Kamati Shirikishi ya Baraza la Mawaziri ikiongozwa na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i Jumapili imesema kuwa mikakati hiyo inalenga kuhakikisha usalama wa wanafunzi wanaporipoti shuleni na watakapoendelea na masomo wakati huu wa janga la Covid-19.

“Tumebuni kituo cha kufuatilia matukio kuhusu ufunguzi wa shule. Kituo hicho kitasimamiwa na Wizara ya Usalama wa Ndani lakini kitashirikisha maafisa kutoka Wizara ya Afya, Elimu na Uchukuzi. Kituo hicho pia kitashirikisha maafisa kutoka Tume ya Huduma za Walimu (TSC), Chama cha Wazazi Nchini (KPA) na vyama vya walimu wakuu katika shule za upili na msingi,” Dkt Matiang’i akasema nje ya jumba la KICC, Nairobi baada ya kuongoza mkutano huo.

Dkt Matiang’i, ambaye alikuwa ameandamana na wenzake, George Magoha (Elimu), Mutahi Kagwe (Afya) na James Macharia (Uchukuzi) alisema kituo hicho maarufu kama “command centre” kitakuwa kikipokea habari zote kuhusu matukio shuleni kuhusiana na maambukizi ya virusi vya corona na kupendekeza hatua za kuchukuliwa haraka.

Shule zinafunguliwa baada ya wanafunzi kusalia nyumbani kwa miezi tisa baada ya mlipuko wa Covid-19 mnamo Machi 13, 2020 nchini Kenya.

“Kando na usalama wa wanafunzi, serikali pia inahimiza walimu na wafanyakazi wengine kuzingatia masharti yote yaliyotolewa na Wizara ya Afya kuzuia mambukizi ya Covid-19 haswa kuvalia barakoa nyakati zote,” akaongeza Dkt Matiang’i .

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na mwenyekiti wa kamati ya elimu katika baraza la magavana Gavana Mutahi Kahiga, Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia, mwenyekiti wa chama cha walimu wakuu wa shule za upili (KESSHA) Kahi Indimuli, mwenzake wa shule za msingi Nicholas Gathemia na mwenyekiti wa KPA Nicholas Maiyo.

Habari zinazohusiana na hii

Mfalme wa Kisii