• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Leicester City wacharaza Newcastle United na kuingia ndani ya mduara wa tatu-bora EPL

Leicester City wacharaza Newcastle United na kuingia ndani ya mduara wa tatu-bora EPL

Na MASHIRIKA

MABAO kutoka kwa James Maddison na Youri Tielemans yalisadia Leicester City kupepeta Newcastle United 2-1 mnamo Jumapili ugani St James’ Park na kupaa hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Chini ya kocha Brendan Rodgers, Leicester kwa sasa wanajivunia alama 32, moja pekee nyuma ya viongozi Manchester United na Liverpool ambao ni mabingwa watetezi wa taji la EPL.

Bao lililofumwa wavuni na Maddison lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Jamie Vardy katika dakika ya 55.

Goli la Tielemans aliyevurumisha kombora kutoka hatua ya 20 lilichangiwa na kiungo mvamizi raia wa Uingereza, Marc Kevin Albrighton kunako dakika ya 72.

Newcastle ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 15 kwa alama 19 walifutiwa machozi na fowadi Andy Carroll dakika nane kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha pili kupulizwa.

Goli la Carroll lilikuwa lake la kwanza kambini mwa Newcastle tangu ajiunge upya na kikosi mnamo Agosti 2019 na lilikuwa lake la kwanza kwa ndani ya jezi za Newcastle tangu 2010.

Ushindi wa Leicester uliwawezesha kuwaruka Tottenham Hotspur na Everton ambao kwa sasa wanajivunia alama 29 kila mmoja. Hata hivyo, masogora hao wa Rodgers wamesakata mchuano mmoja zaidi kuliko Spurs, Liverpool na Man-United ambao wamepiga jumla ya mechi 16 kila mmoja.

Leicester walijibwaga uwanjani kwa minajili ya mchuano huo wakitawaliwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kuambulia sare katika mechi mbili za awali. Kushindwa kwao na Newcastle kungalididimiza matumaini yao ya kusalia katika mduara wa wagombezi halisi wa taji la EPL msimu huu.

Japo Leicester hawakumiliki asilimia kubwa ya mpira katika kipindi cha kwanza, ushirikiano kati ya Vardy, Maddison na Tielemans uliwatatiza pakubwa mabeki wa Newcastle kila mara walipopata mpira na kufanya mashambulizi.

Mchuano dhidi ya Leicester ulikuwa wa tano mfululizo kwa Newcastle kushiriki ligini bila ya kusajili ushindi.

You can share this post!

Kafyu kuendelea

SERIE A: Martinez afunga mabao matatu na kusaidia Inter...