• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Barcelona waponea dhidi ya Huesca katika Ligi Kuu ya Uhispania

Barcelona waponea dhidi ya Huesca katika Ligi Kuu ya Uhispania

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Lionel Messi alichangia bao la pekee lililofungwa na kiungo mkabaji Frenkie de Jong katika ushindi mwembamba wa 1-0 uliosajiliwa na Barcelona dhidi ya Huesca katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumapili.

Mchuano huo ulikuwa wa 750 kwa Messi kuchezea Barcelona na wake wa 500 katika kampeni za kuwania taji la La Liga

Barcelona walitamalaki mchuano na kumiliki asilimia kubwa ya mpira huku kombora la Messi katika kipindi cha kwanza likigonga mwamba wa goli la Huesca waliopoteza nafasi nzuri ya kusawazisha kupitia Rafa Mir mwishoni mwa kipindi cha pili.

Chini ya kocha Ronald Koeman, Barcelona waliingia uwanjani wakitawaliwa na kiu ya kujinyanyua baada ya Eibar kuwalazimishia sare ya 1-1 katika mchuano wa awali ligini.

Mbali na Messi, wanasoka wengine wa Barcelona waliomtatiza kipa Alvaro Fernandez wa Huesca ni Ousmane Dembele na Pedri.

Ushindi wa Barcelona uliwapaisha hadi nafasi ya tano kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 28 huku pengo la pointi 10 likitamalaki kati yao na viongozi Atletico Madrid ambao wana mchuano mmoja zaidi wa kutandaza ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na washindani wao wakuu.

Huesca wangali mkiani mwa jedwali kwa alama 12 kutokana na mechi 17 za hadi kufikia sasa. Ni pengo la pointi tatu ndilo linalowatenganisha na Valencia ambao kwa pamoja na Osasuna (alama 14), pia wamo ndani ya mduara wa vikosi vilivyoko kwenye hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

You can share this post!

Brian Mandela afunga bao na kusaidia waajiri wake Mamelodi...

Ronaldo afungia Juventus mabao mawili dhidi ya Udinese na...