Baadhi ya watumiaji mitandao ya kijamii wakosoa Uhuru kuzidisha kafyu tena

Na JUMA NAMLOLA

WAKENYA na baadhi ya watumiaji mitandao ya kijamii walikosoa vikali hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kuongeza muda wa watu kuingia nyumbani kufikia saa nne za usiku kwa zaidi ya miezi miwili.

Baadhi ya viongozi ambao wamechukua msimamo wa kumuunga mkono Naibu Rais Dkt William Ruto walikuwa mstari wa mbele kukashifu hatua hiyo.

Seneta wa Narok Ledama Ole Kina alishangaa ni kwa nini serikali inaongeza kafyu na kufungua shule.

“Unaongeza muda wa kafyu, unapandisha ushuru, unafungua shule na kisha unatarajia wazazi watakuwa na pesa za kulipia karo,” akaandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Kauli yake ilirejelewa na mbunge wa Kapseret, Bw Oscar Sudi na kuibua maswali mitandaoni kuhusu iwapo mmoja aliiba kauli hiyo kwa mwenzake au la.

Kwenye ukurasa wa Twitter wa Ikulu, Wakenya walionyesha hasira zao na kueleza kuwa hatua ya Rais haitakuwa na umuhimu kwa uchumi wa nchi.

Patriotic Kenyan alidai hakuna lolote litakalotimizwa kiuchumi iwapo nchi itaendelea kutekeleza masharti ya kafyu.

“Kuwapunguzia watu ushuru kulipaswa kuendelezwa sawa na muda wa kufanya kazi pamoja na masaa ya kafyu,” akaandika Ekidor Jnr. @stephenchege94 alimshauri Rais Kenyatta aachane na kafyu, aliyodai inaendelea kuwatajirisha maafisa wa polisi.

“Tafadhali ondoa hii kafyu. Hawa polisi watanunua BMWs na pesa za kafyu.”

Mzee Hustler alitoa malalamishi yake kuhusu masharti ya kufaa barakoa katika eneo ambako hakuna maji. Rais alisema kafyu hiyo itaendelea hadi Machi 21.

Habari zinazohusiana na hii

Uhuru aomba talaka

NDIO! HAPA WIZI TU

Ahadi juu ya ahadi

Huu ni mzaha tu!