• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Mgao wa masomo kufika shule wiki hii

Mgao wa masomo kufika shule wiki hii

Na WAANDISHI WETU

WAZIRI wa Elimu, George Magoha amekariri kuwa fedha za mpango wa elimu bila malipo katika shule za msingi na upili zitatumwa katika taasisi hizo kuanzia Jumanne hadi Ijumaa.

Alikiongea na wanahabari Jumapili nje ya jumba la KICC, Nairobi, Profesa Magoha alisema Sh4 bilioni za shule za msingi ndizo zitawasilishwa kwanza kisha Sh14 bilioni za shule za upili zifike katika akaunti zao kuanzia Ijumaa wiki hii.

“Waziri wa Fedha mwenzangu Ukur Yatani ambaye yuko hapa amenihakikishia kuwa pesa za shule za msingi tayari zimetolewa na zitafikisha shuleni Jumanne. Fedha za shule za upili nazo zitapatikana katika akaunti za taasisi hizo kuanzia Ijumaa,” Profesa Magoha akawaambia wanahabari.

Alisema hayo baada ya kuhudhuria mkutano wa kujadili ufunguzi wa shule ulioongozwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i.

Kando na Waziri Yatani, wengine waliokuwepo ni Mutahi Kagwe (Afya), Joe Mucheru (Maji), James Macharia (Uchukuzi) na Sicily Kariuki (Maji).

Profesa Magoha pia aliwataka wazazi wenye uwezo wa kifedha kulipa karo za watoto huku akikariri kuwa walimu wakuu wasiwafukuze nyumbani wanafunzi watakaoripoti shuleni bila karo.

Alisema wazazi wanafaa kuchangia mahitaji ya watoto wao shuleni jinsi ambavyo wamekuwa wakifanya wakati shule zilikuwa zimefungwa kutokana na janga la Covid-19.

“Ikiwa mzazi amekuwa akilisha mtoto wake nyumbani kwa kwa kipindi hiki chote sioni ni kwa nini mzazi kama huyo hawezi kulipa karo ili walimu wakuu waweze kuwanunulia watoto wao chakula na mahitaji mengine,” akaeleza.

Wakati huo huo, wazazi wengi na wanafunzi katika maeneo mbalimbali nchini walikosa kuhudhuria ibada makanisani jana na badala yake kwenda katika maduka makuu na masoko katika shamrashamra za kutayarisha watoto wa kurudi shuleni leo Jumatatu.

Wazazi katika maeneo mbalimbali ya Lamu walisema miundomsingi duni, ikiwemo uhaba wa madarasa, madawati, vyoo na ukosefu wa maji huenda ukachangia visa zaidi vya Covid-19 kusambaa miongoni mwa wanafunzi na walimu punde shule zitakapoanza kuhudumu nchini.

Ripoti za CHARLES WASONGA, SAMMY KIMATU NA KALUME KAZUNGU

  • Tags

You can share this post!

Madereva kupimwa ulevi, safari za treni kuongezwa

BI TAIFA JANUARI 4, 2021