Vinara wa KRU wakuna vichwa katika juhudi za kufanikisha maandalizi ya wanaraga wa Kenya Simbas kwa minajili fainali za Kombe la Dunia

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) litajitahidi maradufu katika mipango ya kuchangisha fedha ili kuhakikisha kwamba timu ya taifa ya wanaraga 15 kila upande almaarufu Kenya Simbas inafuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Ufaransa mnamo 2023.

Mwenyekiti wa KRU Oduor Gangla amesema kwamba watalazimika kuwa wabunifu zaidi ili kufadhili kikosi cha Simbas kinacholenga kunogesha fainali hizo kwa mara ya kwanza baada ya kuambulia pakavu katika makala mawili ya awali licha ya kuwa pua na mdomo kupata tiketi.

“Itatujuzu kujibidiisha zaidi ili kufanikisha maandalizi ya Simbas kwa minajili ya mechi za kufuzu zitakazoandaliwa kuanzia mwaka wa 2022,” akasema Gangla kwa kufichua kwamba KRU imekuwa ikiwazungumzia wahisani na wadhamini mbalimbali.

Kati ya fedha zitakazochangishwa, Sh20 milioni zitatumiwa kufanikisha ziara ya Simbas nchini Afrika Kusini ambapo wamepangiwa kuvaana na kikosi mseto cha Chuo Kikuu cha Stellenbosch XV mnamo Aprili 2021.

Mechi hizo za kirafiki zitakuwa sehemu ya maandalizi ya Simbas kwa Kombe la Afrika na michuano ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.

Fedha hizo zitatumiwa kwa ajili ya tiketi za safari ya ndege, malazi, malaji na gharama nyinginezo za ziada kwa kipindi cha wiki mbili ambapo kikosi cha Simbas kitakuwa Afrika Kusini.

Simbas walikuwa Afrika Kusini kwa mara ya mwisho mnamo 2014 kuwania taji la Vodacom Cup chini ya kocha Jerome Paarwater aliyewaongoza kukamilisha kampeni za kipute hicho katika nafasi ya saba baada ya kushinda mechi moja pekee na kupoteza sita.

Kocha Paul Odera amesema kwamba ni vyema kwa kikosi cha Simbas kusalia katika hali ya ushindani baada ya kampeni za msimu mzima wa 2020 kufutiliwa mbali kutokana na janga la corona.

Ili kuweka hai matumaini ya kubwaga Stellenbosch, Simbas wamewaajiri wakufunzi wawili raia wa Afrika Kusini – Neil De Kock ambaye ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini almaarufu ‘Springbok’ na Ernst Joubert ambaye ni nahodha wa zamani wa kikosi cha Saracens.

“Mechi za kujipima nguvu dhidi ya Stellenbosch zitatupa jukwaa la kuimarisha baadhi ya idara na kujiweka sawa kwa michuano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia,” akasema Odera.

Ni matumaini ya Odera kwamba Wizara ya Michezo itawapa wanaraga wa Simbas idhini ya kuanza maandalizi mwezi huu wa Januari 2021 ili kujifua vilivyo kwa kipute dhidi ya Stellenbosch.

“Kwa kuwa sasa hakuna mechi za ligi na wanaraga wengi hawajashiriki michezo yoyote kwa takriban miezi tisa iliyopita, tutategemea zaidi wachezaji waliotuwajibikia mwaka uliopita wa 2019-20. Hao ndio tutakaowaita kambini baada ya kupata idhini ya Serikali kupitia KRU,” akaeleza Odera.