• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Kamishna wa Kaunti ya Kiambu azuru Shule ya Mwiki Githurai

Kamishna wa Kaunti ya Kiambu azuru Shule ya Mwiki Githurai

Na LAWRENCE ONGARO

SERIKALI itaendelea kuchunguza jinsi wanafunzi wanavyoendelea kurejea shuleni baada ya miezi tisa wakiwa nyumbani.

Kamishna wa Kaunti ya Kiambu, Bw Wilson Wanyanga alizuru Shule ya Msingi ya Mwiki eneo la Githurai mnamo Jumatatu ili kujionea jinsi wanafunzi walivyokuwa wakirejea shuleni.

Alisema lengo lao ni kuzuru shule kadha ili kujionea wenyewe jinsi wanafunzi wanavyorejea masomoni.

“Tunaelewa kutakuwa na changamoto wanafunzi wote wakisharejea shuleni, lakini serikali itafanya juhudi kukabiliana na changamoto hiyo,” alisema Bw Wanyanga.

Baadhi ya maafisa walioandamana na kamishna huyo ni maafisa wa serikali, wakuu wa shule, na maafisa wa usalama.

Shule ya Mwiki inajulikana kuwa na wanafunzi wapatao 3,551 huku wakiwa katika eneo dogo.

“Serikali itafanya juhudi kuona ya kwamba inashirikiana na walimu ili kukabiliana na janga la Covid-19.

“Tayari nimeridhika na jinsi baadhi ya shule zinavyoendelea kufanya maandalizi yao katika kukabiliana na janga la corona,” alisema Bw Wanyanga.

Alisema shule hiyo tayari imeweka vituo 113 vya maji ya kunawa mikono na tanki za maji ili kutosheleza matakwa ya wanafunzi hao.

Aliongeza kueleza kuwa shule ya Mwiki imepokea madawati 70 yatakayotumika na wanafunzi hao.

Hata hivyo wazazi kadha wamelalamika kuwa wamekuwa wakiulizwa kulipa Sh3,500 za madawati kwa watoto wao wanaojiunga na shule hiyo.

Mzazi mmoja alidai ya kwamba ana watoto wanne na atalazimika kulipa Sh14,000 kwa watoto wote wanne.

Ilidaiwa kuwa kuna madarasa 41 pekee huku kila darasa likiwa na wanafunzi 86.

Bw Wanyanga alisema atachunguza malalamiko hayo ili kubainisha ukweli wake.

Hivi majuzi mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara alitenga Sh7 milioni zitakazotumika kwa ujenzi wa madarasa kadha katika eneo la Gatong’ora.

Kulingana na mbunge huyo, mpango huo utapunguza msongamano unaoshuhudiwa kwa wakati huu katika shule ya Mwiki.

“Kwa muda mrefu wanafunzi na walimu wamekuwa wakipitia hali ngumu katika shule hiyo na kwa hivyo ni vyema kupunguza mzigo huo na kuongeza madarasa mengine zaidi,” alinukuliwa akisema Bw King’ara.

You can share this post!

Ni aibu Magoha kupotosha kuwa ni rahisi kustawisha nchi...

Wanaraga wa Kenya Lionesses waalikwa kwa mechi za kirafiki...