• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Barua ya Kang’ata yawasha moto

Barua ya Kang’ata yawasha moto

BENSON MATHEKA na JUSTUS OCHIENG

BARUA ya Kiranja wa Wengi katika Seneti, Irungu Kang’ata kwa Rais Uhuru Kenyatta akimweleza wazi kwamba, wakazi wa eneo la Mlima Kenya hawataunga kura ya maamuzi kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), imewasha moto huku viongozi wakimlaumu vikali kwa kumhujumu kiongozi wa nchi.

Viongozi wa chama cha ODM ambao wamekuwa wakipigia debe mchakato huo pia walimkashifu Bw Kang’ata wakisema anatumiwa kuchochea wakazi kukataa marekebisho ya katiba yaliyopendekezwa.

Lakini wandani wa Naibu Rais William Ruto ambao wamekuwa wakipinga marekebisho ya katiba yanayoongozwa na Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, walimuunga Bw Kang’ata wakisema hatua yake ni ishara mchakato huo unasambaratika.

Magavana wa kaunti zote za eneo la Mlima Kenya, walijitenga na maoni ya Bw Kang’ata kwamba, viongozi waliochaguliwa wametengwa kwenye mchakato huo, jambo ambalo limeufanya wakazi kutoukumbatia.

Kwenye barua aliyomwandikia Rais Kenyatta Disemba 30 2020, Bw Kang’ata anasema kwamba, BBI sio maarufu eneo la Mlima Kenya.

Magavana Francis Kimemia (Nyandarua), Anne Waiguru (Kirinyaga) Mutahi Kahiga( Nyeri), Kiraitu Murungi (Meru), Lee Kinyanjui (Nakuru), James Nyoro( Kiambu), Martin Wambora (Embu), Ndiritu Murithi (Laikipia), Mwangi wa Iria (Muranga) na Muthomi Njuki wa Tharaka Nithi walimlaumu seneta Kang’ata kwa kudanganya kwamba eneo lao haliungi BBI. Mwenyekiti mwenza wa kamati inayoshughulikia BBI Junet Mohammed alisema kwamba Bw Kang’ata anatumiwa na Dkt Ruto kuvuruga kura ya maamuzi. “Ninavyojua ni kwamba, tunasonga mbele na kwa sasa, saini zinaendelea kukaguliwa,” alisema.

Katibu Mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini (Cotu)Francis Atwoli, alisema kama Bw Kangata angekuwa mwaminifu katika barua yake, hangeitoa kwa wanahabari.

“Nafiriki wako na vita vyao katika eneo lao. Labda waliokuwa viongozi wanawapatia wakati mgumu na wanatarajia Rais Kenyatta awasaidie. Hata hivyo, Bw Kang’ata angeshughulikia suala hilo bila kuhusisha wanahabari,” alisema Bw Atwoli, mmoja wa wanaopigia debe BBI.

Mbunge wa Nyeri Mjini Wambugu Ngunjiri ambaye ni mtetezi wa BBI, alisema Bw Kang’ata hana faida kwa chama cha Jubilee.

You can share this post!

Masaibu tele shuleni

Mkazi wa Nairobi apinga uchaguzi wa ugavana