• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
WASONGA: Serikali ihalalishe mbinu mbadala za masomo janga jingine likitokea

WASONGA: Serikali ihalalishe mbinu mbadala za masomo janga jingine likitokea

Na CHARLES WASONGA

MENGI yamesemwa kuhusu madhara ya janga la Covid-19 katika sekta ya elimu kwa ujumla kufuatia kusitishwa kwa masomo ya kawaida kwa miezi tisa kuanzia Machi 15, 2020 hadi wiki hii.

Kwa mfano, baadhi ya wanafunzi wamerejea shuleni wakiwa na msongo wa kiakili baada ya wazazi wao kufariki kutokana na ugonjwa huu huku wengine wa kike wakigeuka “wazazi” baada kutungwa mimba za mapema.

Watoto hao wa kike, haswa wale kutoka jamii masikini, walipata uja uzito kwa sababu serikali haikuweka njia mbadala ya wao kuweza kuendelea na masomo baada ya shule kufungwa.

Jaribio la Serikali, kupitia Wizara ya Elimu, la kuanzisha masomo kupitia mitandaoni, redio na kwenye runinga, halikufua dafu kwani yaliwafungia nje idadi kubwa ya wanafunzi kutoka jamii masikini ambao wazazi wao hawawezi kumudu mitambo hiyo ya kisasa.

Mpango wa elimu ya kijamii ambao serikali ilianza mnamo Julai mwaka jana pia haukufaulu baada ya watu fulani kuwasilisha kesi kortini kupinga uhalali wake.

Kwa hivyo, lingekuwa jambo la busara iwapo serikali ingetumia ujio wa janga hilo la Covid-19 kama nafasi ya kubuni njia mbadala, na halali, za kuwezesha wanafunzi wote kuendelea na masomo yao pasi kutatizika endapo masomo ya kawaida yatasitishwa tena siku zijazo yalivyofanyika Machi 15, mwaka jana.

Kwa mfano, serikali inapasa kubadilisha sheria husika za elimu ili kuhalalisha mafunzo kupitia mitandaoni. Hii ni kwa sababu ilivyo sasa mafunzo hayo hayatambuliwi kisheria kuwa mbinu mbadala ya kufanikisha utekelezaji wa mitaala, haswa katika shule za msingi na upili.

Ndiposa japo, baadhi ya wanafunzi walikuwa wakiendelea na masomo mitandaoni, redioni au kupitia runinga, shule zilipofunguliwa wiki hii, walimu walianza kutekeleza mitaala mahala ambapo waliachia Machi 15, 2020 ili kufidia muda uliopotezwa.

Ili kufanikisha mpango wa masomo mitandaoni, serikali inapasa kufufua mpango wa masomo ya kidijitali kuanzia katika kiwango cha shule za msingi hadi vyuo vikuu.

Ikumbukwe kwamba endapo serikali hii ya Jubilee ingefanikisha mpango wa usambazaji vipakatalishi kwa wanafunzi wa darasa la kwanza, kuanzia 2013 ilipoinga mamlakani, wanafunzi wote ambao wakati huu wako katika daraza la nane wakati huu wameendelea na masomo barabara nyakati za janga la Covid-19. Hata hivyo, mradi huo ulikwama.

Kwa hivyo, ndio wakati mwafaka kwa wapanga sera katika wizara ya elimu, wakiongozwa na Waziri Profesa George Magoha, kuketi na kujadili njia za kufufua elimu ya dijitali katika shule za msingi.

Wabunge nao wapitishe sheria za kuhalalalisha mafunzo kupitia mbinu hii na nyinginezo zinazoendana na mahitaji ya nyakati hizi.

[email protected]

You can share this post!

Mkazi wa Nairobi apinga uchaguzi wa ugavana

BI TAIFA JANUARI 5, 2021