TAHARIRI: SGR iwape abiria huduma kisiwani

KITENGO CHA UHARIRI

SHIRIKA la Reli Nchini (Kenya Railways) hatimaye limeanzisha huduma ya uchukuzi wa treni nyakati za usiku kati ya Nairobi hadi Mombasa kupitia reli ya kisasa (SGR).

Kwenye notisi iliyotumwa kwa vyombo vya habari, treni hizo mbili za Madaraka Express zitaondoka vituo vya Nairobi na Mombasa saa tatu za usiku na kusimamama katika vituo saba vilivyoko kati ya miji hiyo miwili.

Abiria watakuwa wakiruhusiwa kushuka katika vituo vya treni saa za kafyu na kuelekea sehemu nyinginezo, mradi watoe ithibati ya tiketi endapo kwa maafisa wa usalama. Hapo awali, Madaraka Express imekuwa ikiendesha huduma za treni mbili kati ya miji hiyo miwili (Nairobi na Mombasa), safari zikianza saa mbili asubuhi na saa tisa alasiri.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la KRC Philip Mainga alieleza kuwa huduma za treni hizo mbili zitawafaa wasafiri ambao watakosa usafiri wa magari ya abiria.

Hii ni hatua nzuri kwa kuwa ingawa nchini inaendelea kutekeleza amri ya kafyu, wanaosafiri kati ya miji hiyo miwili watakuwa wakiondoka kabla ya kafyu na kuwasili baada ya kafyu.

Tangu kusimamishwa kwa safari za usiku, wafanyibiashara na watu wengine wenye shughuli muhimu wamekuwa wakiteseka sana. Kuna wauzaji samaki ambao walikuwa wakiondoka na samaki wao Mombasa usiku, na kuwafikisha katika msoko kama City Market jijini Nairobi asubuhi.

Sasa hivi biashara hiyo haiendelei ipaswavyo kwa kuwa samaki wanaposafirishwa mchana, kuna uwezekano mkubwa kwamba wengi wataoza.

Kuanzishwa kwa safari hizi za usiku kusiwe ni majaribio pekee wakati huu ambapo kuna wasafiri wengi kutokana na shamrashamra za Krismasi na Mwaka Mpya.

Aidha, Shirika la Reli lapaswa kufikiria kuanzisha huduma za garimoshi kati ya kituo kikuu cha Miritini na kile kilichoko katikati ya mji wa Mombasa. Garimoshi hilo litavutia watu wengi kusafiri usiku, kwa kuwa watakuwa wanafikishwa ndani ya mji, kama inavyofanyika kwa wenzao wanaobebwa kutoka Syokimau.

Kwa sasa kituo cha Mirini hakina sehemu ya watu wanaotoka Nairobi kusubiri kupambazuke. Wanapofika kituoni, huanza kutafuta usafiri wa kuwafikisha wanakoenda.

Kuwafikisha abiria saa tisa za usiku huenda kukashawishi wahalifu kuwategea njiani. Itakuwa vyema kama watakuwa wakibebwa hadi katikati ya jiji, wanakoweza kupata usafiri salama wa kutegemewa.

Habari zinazohusiana na hii