• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Barua kwa Rais: Kang’ata aomba msamaha

Barua kwa Rais: Kang’ata aomba msamaha

Na CHARLES WASONGA

KIRANJA wa wengi katika Seneti Irungu Kang’ata sasa anadai kuwa barua aliyomwandikia Rais Uhuru Kenyatta akisema kwamba mpango wa maridhiano (BBI) hauna umaarufu eneo la Kati mwa Kenya ilitolewa kwa vyombo vya habari na mtu mwingine.

Hata hivyo, Seneta huyo wa Murang’a anashikilia kuwa masuala yote yali kwenye barua hiyo ni za kweli, akisema ni matumaini yake kwamba yatashughulikiwa.

“Ingawa barua hiyo iliyoandikwa mnamo Desemba 30, 2020 ni halali, sikuwasilisha nakala yake kwa vyombo vya habari; ni mtu mwingine niliyemtumia nakala yake. Naomba radhi kwa hilo. Ukweli ni kwamba sikupaswa kutuma nakala yake kwa mtu mwingine. Naamini kuwa masuala mazito yaliyoibuliwa katika barua hiyo yatashughulikiwa,” akasema Bw Kang’ata Jumatatu.

Katika barua hiyo iliyoangazia masuala mengi, seneta huyo anasema uchunguzi wake umebaini kuwa ni watu wawili kati ya 10 pekee katika eneo la Mlima Kenya wanaunga mkono BBI.

Bw Kang’ata alisema alifanya uchunguzi huo wakati wa msimu wa sherehe za Krismasi.

Vile vile, kiranja huyo wa wengi katika seneti alimwambia Rais Kenyatta kwamba huenda mgombea wa Jubilee katika uchaguzi mdogo ujao wa ugavana wa Nairobi akabwagwa.

Alisema matokeo kama hayo yataathiri pakubwa ajenda ya serikali katika Bunge la Kitaifa na lile la Seneti.

Barua hiyo ilizua cheche miongoni mwa viongozi wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya huku magavana 10 wakiipuzilia mbali.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa kundi la magavana wa Mlima Kenya Francis Kimemiah (Gavana wa Nyandarua) walitaja hatua ya seneta huyo kumwandikia Rais Kenyatta barua ya wazi kama iliyokiuka itifaki.

“Kama kiongozi mwenye cheo kikubwa katika seneti na chama cha Jubilee, Seneta Kang’ata alifaa kufuata taratibu rasmi za serikali kuwasiliana na Rais Kenyatta. Huu ni ukiukaji wa itifaki na hauwezi kukubaliwa. Mbona kiongozi kama huyu aamue kuwasiliana na Kiongozi wa Taifa kwa njia isiyo ya heshima jinsi hii?”taarifa hiyo ikasema.

Waliungama kuwa japo baadhi ya masuala ambayo Bw Kang’ata aliibua yana mashiko “ni mapema kubaini ikiwa mswada wa BBI utapita au la.”

Miongoni mwa magavana waliotia saini taarifa hiyo ni; Kiraitu Murungi (Meru), Mutahi Kahiga (Nyeri), Lee Kinyanjui (Nakuru) na Mwangi wa Iria (Murang’a).

You can share this post!

ONYANGO: IEBC ielekeze jinsi ya kuendesha kampeni za...

SHINA LA AFYA: Ugonjwa wa ‘kusikia sauti kichwani’...