TAHARIRI: Serikali ilipaswa kuboresha shule

KITENGO CHA UHARIRI

MNAMO Jumatatu, wanafunzi wote walirejea shuleni baada ya kuwa nje kwa karibu mwaka.

Japo ugonjwa wa corona ungalipo, serikali kupitia Waziri wa Elimu Prof George Magoha, iliwahakikishia wazazi usalama wa watoto wao shuleni.

Alisema kulikuwa na maandalizi ya kutisha. Hata hivyo, matukio yanayoendelea kushuhudiwa shuleni kote nchini yanadhihirisha kuwa serikali haikuwa imejiandaa vyema kwa ufunguzi wa shule. Ahadi ya kujenga madarasa haikutekelezwa katika shule nyingi ambazo zimesalia na miundomsingi tu yao ya zamani.

Changamoto zaidi ni kwamba baadhi ya shule bado zimejaa maji ya mafuriko na wanafunzi wao kulazimika kuungana na wenzao katika shule jirani ambazo hazikuathirika.

Suala hili limeleta msongamano mkubwa kwenye shule hizo huku wizara nayo ikikosa kutoa fedha za kugharamia madarasa ya ziada.

Mfano halisi ni shule ya msingi Kandaria katika eneobunge la Nyando, Kaunti ya Kisumu ambayo wanafunzi wake wamelazimika kusomea pamoja na wenzao katika shule ya msingi ya Ugwe japo madarasa hayatoshi.

Kinyume na nchi yetu, Rwanda ambayo pia iliathirika na virusi vya corona, ilipiga hatua katika kujenga madarasa, kuongeza madawati na kuimarisha miundomsingi shuleni na sasa wanafunzi wao wanasoma bila hofu zozote.

Ni kweli kwamba serikali ilitoa madawati katika shule mbalimbali nchini, lakini madawati hayo hayatoshi kukidhi idadi ya wanafunzi inayohitajika kutimiza hitaji la kuketi umbali wa mita moja unusu shuleni kuzuia corona.

Japo masomo hayafai kukatizwa, huu ndio wakati ambapo serikali inafaa kutumia aslimia kubwa kwenye bajeti yake kugharimia ujenzi wa madarasa mengine shuleni. Pia yapaswa kununua ardhi ambako shule zilizoathiriwa na mafuriko zitajengwa upya.

Kulingana na jinsi hali ilivyo, ni dhahiri kuwa wanafunzi wetu wako katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona. Ni vyema walimu wahakikishe kuwa masharti yaliyowekwa na wizara ya Afya yanafuatwa hata katika mazingira magumu.

Pia serikali za kaunti zihakishe kuwa shule nyingi zina maji. Hii ndiyo njia itakayowezesha shule hizo kutimiza viwango vya juu vya usafi.

Habari zinazohusiana na hii